Mufuruki aibua jina jipya la biashara ya mkaa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mazingira ya Taifa Tanzania, Ally Mufuruki akitoa mada katika mjadala wa Jukwaa la Frika linalojadili matumizi ya mkaa, uchumi na mazingira yetu, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Kuhifadhi  Mazingira, Ali Mufuruki, ameibua  jina jipya la biashara ya mkaa akisema ni “biashara shenzi.”

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Kuhifadhi  Mazingira, Ali Mufuruki ameibua  jina jipya la biashara ya mkaa akisema ni “biashara shenzi.”

Ameibua jina hilo leo Alhamisi Februari 7, 2019 wakati akizungumza katika mdahalo wa  Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL).

Katika Jukwaa hilo la tatu kuendeshwa na MCL lenye mada ya  mkaa, uchumi na mazingira linalofanyika katika ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam usiku huu, Mufuruki amesema kuendelea kuruhusu biashara hiyo ni sawa na kujiua wenyewe.

Amesema biashara hiyo ni ‘shenzi’ kwa kuwa ina athari  kubwa kuliko faida na endapo Serikali itaruhusu iendelee, itaiangamiza nchi.

“Biashara ya mkaa kwa athari hizi ni biashara shenzi tunajiua wenyewe, ni biashara ambayo haitolewi  kodi haina faida, ni sumu ni sawa na kufanya biashara ya ukahaba na kudai kodi,” amesema na kuibua vicheko miongoni mwa wananchi waliohudhuria mdahalo huo.

Hata hivyo, Mufuruki ametupa lawama kwa Serikali kwa kuendelea kutoza kodi katika biashara hiyo bila kujali athari zake kwa mazingira.

“Serikali inatoa mix massage (ujumbe tofauti) watu wanasema tunaenda kufanya biashara  tutoze kodi, wengine wanasema tupande miti, huwezi kupanda miti na kuuvuna ukiwa hai," amesema Mufuruki.