VIDEO: Muongoza watalii ajirusha mlima Kilimanjaro, afariki dunia

Muktasari:

Thomas Meela (58), mkazi wa Marangu anayejishughulisha  kuongoza watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro amekufa baada ya kujirusha kwenye kilele cha mlima huo umbali wa mita 5,895


Moshi. Thomas Meela (58), mkazi wa Marangu anayejishughulisha  kuongoza watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro amekufa baada ya kujirusha kwenye kilele cha mlima huo umbali wa mita 5,895.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 17, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema tukio hilo limetokea Septemba 15, 2019 katika hifadhi ya mlima huo.

Amesema huenda Meela alichanganyikiwa baada ya kupata ‘homa ya mlima’, kuamua kujirusha na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

“Meela alikuwa na safari ya siku tisa kupanda mlima Kilimanjaro na Septemba 12 mchana baada ya kufika kileleni aliwaacha wageni na kwenda kuvuta sigara lakini akiwa na mwenzake ndipo alipomwambia hawatamuona tena.”

“Mwenzake alikwenda kutoa taarifa kwa watu aliokuwa nao ili wampe msaada, waliporudi walikuta amekimbia na tayari ameshajirusha kilele cha uhuru na kuangukia miamba, " amesema.

Kamanda Issah amesema mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC kwa uchunguzi.