Mvua kubwa kunyesha mikoa tisa Tanzania

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa siku tano kuanzia leo Ijumaa Januari 31, 2020 na kutoa tahadhari kwa wakazi wa mikoa itakayonyesha mvua hizo kuchukua hatua.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalia la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Januari 31, 2020 na TMA imesema athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kesho Jumamosi Februari 1, 2020 TMA imetoa tahadhari  ya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Singida, Dodoma pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

“Angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,” imesema taarifa hiyo

Jumapili ya Februari 2, 2020 TMA imetoa angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Singida, Morogoro, Lindi, Mtwara, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Mara.