Mwanafunzi darasa la nne adaiwa kujinyonga hadi kufa

Friday August 23 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Osanyui jijini Arusha, Eribariki Lekini (12) anadaiwa kujinyonga hadi kufa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amethibitisha kutokea tukio hilo, kubainisha kwa mtoto huyo alijinyonga juzi saa 11 jioni kwa kutumia kamba ya katani.

Amebainisha kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa ukining'inia katika nyumba ya Emmanuel Thomas inayoendelea kujengwa.

"Tunaendea na uchunguzi wa tukio hili kwa sababu huyu mtoto alitumia eneo ambalo ujenzi unafanyika kufunga kamba juu ya dari,” amesema.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Murieti,  John Nanyaro amesema hadi sasa hawajui sababu ya mtoto huyo kujiua.

"Mtoto huyu amekutwa amekufa sasa haijulikani ni kweli amejinyonga ama la ila polisi walichukua mwili na wanachunguza,” amesema. 

Advertisement

Tukio hilo limeibuka ikiwa zimepita siku nne tangu Faisal Salum (19) kujiua kwa kujipiga risasi akidaiwa kutumia bunduki ya baba yake aina ya Rifle Winchester inayoshikiliwa polisi kwa uchunguzi.

 


Advertisement