Mwanaharakati aunganishwa kesi ya ukomo wa urais Tanzania

Mahakama Kuu ya Tanzania

Muktasari:

Mtu mwingine ameunganishwa katika kesi ya kikatiba inayohoji ukomo wa urais iliyofunguliwa Mkulima Patrick Dezydelius Mgoya hivyo kufikisha idadi ya watatu walioomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo itakayoanza kusikilizwa Februari 10, 2020..

 

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imeridhia maombi ya mwanaharakati wa haki za watu wasiojiweza, Mhina Michael Shengena kuunganishwa katika kesi ya kikatiba inayohoji ukomo wa urais na hivyo kuungana na Mkulima Patrick Dezydelius Mgoya.

Uamuzi wa kuridhia maombi ya mwanaharakati huyo kuunganishwa katika kesi hiyo ulitolewa jana Alhamisi Desemba 12, 2019 na Jaji Kiongozi, Eliezer Feleshi ambaye ni mwenyekiti wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo ya msingi ya ukomo wa urais.

Jaji Feleshi alifikia uamuzi huo, baada ya Serikali ya Tanzania kuamua kuondoa dhamira yake ya kutaka kumwekea pingamizi ili asiunganishwe na badala yake ikaamua kukubaliana na maombi hayo.

Shengena ni mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali iitwayo Co-operation for Assisting Handcapped People Tanzania inayojihusisha na utoaji wa huduma ya kuwasaidia watu wasiojiweza kama vile yatima, walemavu na watoto walioko katika mazingira magumu na hatarishi katika sekta za elimu na Afya.

Shengena aliwasilisha maombi hayo namba 55 ya mwaka 2019 mahakamani hapo, akiomba kuunganishwa katika kesi hiyo upande wa mdai ambayo yalitajwa kwa mara ya kwanza Novemba 22, 2019.

Ingawa mjibu maombi wa kwanza, Mkulima Mgoya aliieleza mahakama hana pingamizi, lakini mjibu maombi wa pili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania(AG), kupitia kwa Wakili wa Serikali, Yohana Marko, aliomba wapewe siku 14 ili wawasilishe kiapo kinzani.

Jaji Feleshi alikubaliana  na maombi hayo ya Serikali ya Tanzania na kumwamuru AG kuwasilisha kiapo chake kinzani kabla au Desemba 5, 2019 na akapanga maombi hayo yasikilizwe jana Alhamisi.

Hata hivyo, mpaka jana Alhamisi Serikali ilikuwa haijawasilisha kiapo chake kinzani na maombi hayo yaliyoitwa kwa ajili ya usikilizwaji, Wakili Marko aliieleza mahakama baada ya kupitia sheria zilizotumika katika kuwasilisha maombi hayo wameona hawana sababu ya kuwasilisha kiapo kinzani.

“Kwa hiyo mna-conceed?”, alihoji Jaji Feleshi na Wakili Marko akajibu; “ndio mheshimiwa.”

Baada ya maelezo hayo ya wakili wa Serikali, Jaji Feleshi alimuuliza Shengena kama alikuwa na jambo lolote la kusema lakini akasema hana, kisha Jaji Feleshi akamuuliza mjibu maombi wa pili, Mkulima kama ana lolote la kusema naye akajibu kuwa hakuwa na la kusema.

Baada ya kusikiliza pande zote ndipo Jaji Feleshi akatoa amri ya mwanaharakati huyo kuunganishwa rasmi katika kesi hiyo upande wa Mkulima.

“Kwa kuwa wajibu maombi wote hawapingi maombi haya, ruhusa inatolewa kwa mleta maombi (Shengena) kuunganishwa katika kesi ya msingi namba 19 ya mwaka 2019.”, alisema Jaji Feleshi.

Kesi hiyo namba 19 ya mwaka 2019 aliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mgoya anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya Ibara ya 40(2) ya Katiba ya Nchi.

Ibara hiyo inaweka ukomo wa mtu kuchaguliwa kuwa rais kwa mujibu wa ibara hiyo mtu hataweza kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka  mitanomitano tu yaani miaka 10.

Mgoya anadai masharti ya ukomo yanayowekwa chini ya ibara hiyo yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria  chini ya Ibara ya 13, 21 na 22(2).

Hata hivyo Serikali kupitia kwa AG tayari imeshamwekea pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na mambo mengine ikidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na kwamba kesi hiyo ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Kesi hiyo ya msingi imepangwa kusikilizwa pingamizi la Serikali Februari 10, 2020. Mbali na Jaji Feleshi, majaji wengine katika jopo la majaji wanaoisikiliza ni  Benhajj Masoud na Seif Kulita.

Hadi sasa taasisi mbili moja ya kisiasa yaani Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo) na nyingine ya kisheria yaani Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), nazo zimeshaunganishwa kwenye kesi hiyo, baada ya maombi yao kukubaliwa.

Wakati Shengena akiunganishwa upande wa Mkulima, ACT-Wazalendo na TLS zimeunganishwa kama wadaiwa wenye maslahi katika kesi hiyo.