Mwenyekiti Halmashauri, madiwani wawili waikimbia Chadema, Mbunge afurahia

Friday February 14 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Ziara za Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally zimeendelea kuzibomoa ngome za upinzani baada ya kuwapokea viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Kati ya waliojiunga na CCM jana Alhamisi Februari 13, 2020 na kupokelewa na Dk Bashiru ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mashaka Mbilinyi anayetokana na Chadema.

Wengine ni madiwani, Chiza Shungu (Mbasa), Digna Nyangile (Viti maalum) na kamanda wa Red Briged, Antony Mwampunga na Baraka Masala.

Baada ya kujivua uanachama huo, Dk Bashiri aliwakabidhi kadi za CCM. Mtendaji mkuu huyo wa chama tawala yuko mkoani Morogoro kwa ziara ya siku tatu kuanzia jana.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka alisema wanachama hao wameamua kujiunga na chama hicho baada ya kuridhika na utendaji kazi wa CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.

Shaka alisema kutokana na kazi kubwa inayofanya na CCM wapinzani wengine wamekuwa na shauku ya kujiunga nacho.

Advertisement

Katika ziara hiyo ya jana, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Gertrude Lwakatale alikabidhi pikipiki 22 kwa ajili ya chama hicho mkoani humo zenye lengo la kutumika katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020 pindi zitakapoanza.

Lwakatale ambaye ni Mchungaji Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni  Dar es Salaam alisema tayari alikwisha baiskeli 300 kwa chama hicho ikiwa na nia ya kukisaidia katika kuleta maendeleo ya chama ndani ya jimbo lake.

Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali alifurahishwa na uamuzi huo akisema, “wamefanya jambo zuri kwani kama huyo mwenyekiti wa halmashauri, majuzi madiwani wa CCM na wawili wa Chadema waliandika barua kwa mkurugenzi wakitaka kuitishwa kikao cha baraza ili kumvua uenyekiti.”

“Lakini jana huyohuyo waliyemkataa amekwenda kuungana nao, kwanza nimefurahi kwa sababu angenipa wakati mgumu kumpigania asing’olewe na atakuwa amekwenda kwa kuwakomoa kuwa si mlitaka kuning’oa sasa nakuja kuungana nanyi,” amesema

Mbunge huyo amesema, “kilichofanyika kwangu na chama hakina athari kwa sababu chama ni kikubwa kuliko mtu na mimi na chama ndiyo tuliwaombea kura sasa wajiandae kwenye uchaguzi, nitawapiga kama nilivyowapiga mwaka 2015, hakuna kura yangu itakayoibiwa.”

Lijualikali amesema Mwampunga alifukuzwa uanachama mwaka 2019 na kuhamia CCM, “na picha zipo, sasa jana tena mtu huyo huyo kajiunga na CCM, sasa najiuliza imekuwaje mtu aliyefukuzwa akahamia CCM, jana tena anahamia CCM, haya ndiyo mambo yanayoshangaza.”

Advertisement