Mwenyekiti UVCCM afafanua kauli yake, ampinga aliyetaka wapinzani kuuawa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) nchini Tanzania, Kheri James ametoa ufafanuzi wa  kauli aliyoitoa kuhusu wanachama wa vyama vya upinzani kudekezwa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) nchini Tanzania, Kheri James ametoa ufafanuzi wa  kauli aliyoitoa kuhusu wanachama wa vyama vya upinzani kudekezwa.

James ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 3, 2020 alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kauli aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano mkoani Arusha kuwa vijana wa CCM hawapo tayari kuona wanasiasa wanaodaiwa kuchafua Taifa kuendelea kudekezwa bila hatua zozote kuchukuliwa.

Wakati James akieleza hayo, mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Kenoni Kihongosi alinukuliwa akimzungumzia kiongozi mmoja wa upinzani nchini Tanzania  kwamba kama  angekuwa mkazi wa Iringa asingekuwa salama na kudai kuwa wanasiasa wanaodaiwa kuchafua Taifa wanatakiwa kuuawa.

Hivi karibuni James aliwahi kunukuliwa akisema Serikali ya CCM haiwezi kupeleka maendeleo katika majimbo ya upinzani.

James amelieleza Mwananchi kuwa viongozi wengi wa upinzani wamekuwa wakiendekezwa kufanya upotoshaji bila kuchukuliwa hatua na vyombo husika.

Amesema alichokimaanisha katika hotuba yake ni kushangazwa na utamaduni wa wapinzani kuichafua Tanzania bila kuchukuliwa hatua na vyombo vya dola.

 “Kuna kipindi walizusha CAG Profesa Mussa Assad (amestaafu) katekwa, walichukuliwa hatua? Ule uvumi wa rais wetu walichukuliwa hatua?  Sasa sisi tutaingia kwenye mapambano kwa hoja, wakienda kutuchafua nje, tutawafuata huko huko,” amesema  James huku akikiri kauli za viongozi zinaweza kuhatarisha amani.

Ameongeza, “amani ya nchi hii imeshikiliwa na sisi viongozi, tukichochea uongo tutaharibu nchi hii. Alichokizungumza mwenyekiti wa Iringa siyo msimamo wa UVCCM na tunakemea kauli za aina hiyo, sisi msimamo wetu ni kuhimiza utekelezaji wa misingi ya kisheria.”

 Licha ya vijana wa UVCCM kutoa kauli tata, hata baadhi ya vijana wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) nao wamekuwa wakitao kauli mbalimbali mitandaoni, kuibua mjadala.

Akizungumzia suala hilo mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu amekiri kujitokeza kwa dosari hiyo kwa kiwango kidogo kwa vijana wa chama hicho, na kushangazwa na uongozi wa CCM kutowachukulia hatua vijana wa chama hicho tawala.

“Hatuna kesi nyingi sana ya kauli za uchochezi, na bado hatujawa na plan (mpango), hata baraza lililopita kesi hazikuwa nyingi lakini kama polisi na CCM hawatoi tamko lolote kuhusu kauli za UVCCM maana yake wanabariki, “ amesema Pambalu huku akiwataka vijana kulinda amani ya nchi hii.

“Tunatakiwa kutambua kwamba, kauli za uvunjifu wa amani sio tu zinahatarisha wale unaowalenga katika siasa, ila hata yule aliyetoa kauli hatabaki salama endapo machafuko yakitokea.”

Alipoulizwa kuhusu kauli hizo, msemaji wa polisi, David Misime aliomba kupatiwa muda ili kujiridhisha na kauli zilizotolewa na vijana wa vyama hivyo.