Mwenyekiti wa Chadema halmashauri Arusha ahamia CCM

Aliyekuwa Meya wa jiji la Arusha,Kalisti Lazaro akipokewa rasmi CCM na katibu itikadi na Uenezi wa CCM Taifa,Humphrey Polepole  viwanja vya Mbauda katika jiji la Arusha ambapo CCM imefunga rasmi kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Muktasari:

Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha (Chadema), Noah Lembrice na diwani wa Olmoti, Robert Laban wamehamia CCM leo Jumamosi Novemba 23, 2019.


Arusha. Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha (Chadema), Noah Lembrice na diwani wa Olmoti, Robert Laban wamehamia CCM leo Jumamosi Novemba 23, 2019.

Lembrise ambaye alikuwa diwani wa Oltumet na mwenzake wamejiunga na chama hicho tawala katika mkutano uliofanyika uwanja wa Mbauda na kuhudhuriwa na katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.

Akizungumza katika mkutano huo, Lembrice amesema amejiuzulu kutokana na kutambua kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Kwa upande wake, Polepole amewapongeza wawili hao kwa kujiunga CCM, kwamba kabla ya kuwapokea alishauriana na viongozi wa juu wa chama hicho waliobariki suala hilo.

Kuhama kwa madiwani hao ni pigo jingine la Chadema ndani ya siku tatu kwani Novemba 20, 2019 aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha kwa tiketi ya chama hicho, Calist Lazaro alijiunga CCM.

Lazaro alijiunga CCM na kupoteza nafasi zake za udiwani, umeya, uenyekiti wa mameya na madiwani wa Chadema na ujumbe wa kamati kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kufuatia uamuzi wa Lazaro, Halmashauri ya Jiji la Arusha imebaki na madiwani 33, kati yao 25 wakiwa wa Chadema na wanane CCM.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, CCM ilipata diwani mmoja wa kuchaguliwa katika jiji hilo lakini baadaye kwa nyakati tofauti madiwani saba walijiuzulu Chadema na kujiunga na chama hicho ambako waligombea na kuchaguliwa tena.