Mwili mkurugenzi wa zamani wa Katani Limited kuzikwa kesho Dar

Muktasari:

Mwili wa mkurugenzi mtendaji wa zamani wa kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte aliyefariki Dunia leo alfajiri utazikwa kesho Jumanne Machi 31, 2020 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam.

Tanga. Mwili wa mkurugenzi mtendaji wa zamani wa kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte aliyefariki Dunia leo alfajiri utazikwa kesho Jumanne Machi 31, 2020 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo mchana na msemaji wa familia, Jaji mstaafu John Mkwawa msiba wa Shamte upo nyumbani kwake Mbweni, jijini Dar es Salaam.

"Maziko ni kesho saa 10 jioni katika makaburi ya Kisutu. Msiba upo nyumbani kwake Mbweni,” amesema Jaji Mkwawa.

 Mwananchi ilifika nyumbani kwa marehemu mtaa wa Bombo jijini Tanga na kukuta waombolezaji  wakifanya maandalizi ya kuelekea jijini Dar es salaam.

Shamte alifariki dunia katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu.