Mwili wa Ali Mufuruki kuwasili Tanzania leo jioni

Monday December 9 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Isamil Mufuruki, baba mdogo wa bilionea maarufu nchini Tanzania, Ali Mufuruki aliyefariki dunia jana alfajiri Jumapili Desemba 8, 2019 amesema mwili wa mfanyabiashara huyo utawasili nchini kati ya saa 9:30 alasiri hadi saa 10 jioni ukitokea Afrika Kusini.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 9, 2019 amesema baada ya mwili  wa mmiliki na mwenyekiti  wa kampuni ya Infotech Investment Group kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),  utapelekwa nyumbani kwa ajili ya ibada na kuhifadhiwa katika msikiti wa Mmaamur Upanga jijini Dar es Salaam.

Mufuruki aliyeacha watoto wanne amefariki dunia jana alfajiri katika hospitali ya Morningside jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.

Isamil amesema awali walipanga mwili  kuhifadhiwa Hospitali ya Jeshi Lugalo lakini familia imeamua uhifadhiwe msikitini.

"Mwili unawasili leo utakuja hapa nyumbani kwa ajili ya dua na kisha tutakwenda kumhifadhi msikitini na kesho Jumanne ataagwa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere,” amesema Isamil bila kufafanua maziko yatafanyika wapi na lini.

"Kwa leo tuishie hapa, hatua ya kwanza mwili utakuja na utaagwa lakini wapi akazikwe familia itakaa tena kikao na tutatoa taarifa wapi na lini atazikwa. Kwa sasa tunamsubiri mke wake pamoja na watoto waliopo  Canada,  taarifa zote tutatoa kesho.”

Advertisement

Advertisement