Mwili wa Katibu wa Chadema Wilaya ya Manyoni wakutwa barabarani

Wednesday February 26 2020

 

By Sharon Sauwa na Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mwili wa Katibu wa Chadema Jimbo la Manyoni Mashariki, Alex Jonas umekutwa barabarani ukiwa na majeraha yanayoonyesha amechomwa na kitu chenye ncha kali.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 26, 2020, Katibu wa Chadema Mkoa wa Singida, Samwel Maron amesema taarifa za ilikuaje tukio hilo zitatolewa baadaye na chama mara baada ya kupata taarifa.

“Yeye anaishi nje kidogo na mji wa Manyoni. Hakuna anayejua taarifa zaidi kuhusu alikwenda kufanya nini katika mji huo wala jinsi lilivyotokea bali mwili wake ulikutwa na majeraha ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali,”amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa amesema kuwa tukio hilo lipo na kwamba bado Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi.

“Ni kweli kuna tukio la Katibu wa Chadema Wilaya ya Manyoni kukutwa amefariki dunia leo asubuhi lipo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kutoa taarifa kamili,”amesema.

Mwangisa amesema yeye yupo kwenye kikao mkoani Singida lakini taarifa hizo amezipata na kwamba baadaye watatoa taarifa zaidi ya tukio hilo.

Advertisement

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Singida, Sweetbert Njewike amesema amesikia tukio hilo lipo japo hajajua kama ni kiongozi huyo aliyefariki au ni nani.

Kamanda huyo ameahidi kutoa taarifa zaidi juu ya tukio hilo.

Advertisement