Mzozo wa NBA, China wazidi kukua, Apple yaonywa

Muktasari:

Serikali ya China imezuia tamasha lililoandaliwa kwa ajili ya mashabiki wa mpira wa kikapu baada ya bosi wa klabu ya Houston Rockets kuunga mkono harakati za demokrasia Hong Kong


Shanghai, China (AFP). China leo imeshutumu utetezi wa kamishna wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), Adam Silver kuhusu uhuru wa kuzungumza, ikifuta tamasha la mashabiki wa mchezo huo na kumshambulia katika vyombo vya habari vya serikali.

Wakati hayo yakitokea, Apple imeonywa kuwa inaweza kuwa kampuni nyingine itakayoadhibiwa kwa kuunga mkono waandamanaji wanaotaka demokrasia Hong Kong.

NBA imekuwa ikitegemea kukuza umaarufu wake katika soko kubwa la China wiki hii kwa kuweka mechi mbili za kirafiki za kujiandaa kwa msimu, lakini mipango hiyo ilitibuliwa na ujumbe uliotumwa na meneja mkuu wa klabu ya Houston Rockets, Daryl Morey ukiunga mkono harakati za demokrasia zinazoendelea Hong Kong.

Awali Silver na NBA walijibu ujumbe huo katika mtandao wa Twitter kwa kutoa taarifa ambayo wanasiasa wa Marekani waliielezea kuwa ni kujisalimisha kwa China.

Lakini Silver, ambaye yuko Japan kwa ajili ya mipango mingine ya mechi za kujiandaa kwa msimu zinazoihusu Rockets, baadaye aliichokoza China Jumanne aliposema NBA inaunga mkono uhuru wa kujieleza.

"Maneno ya Silver ni kuhusu taswira, ambayo itawapa nguvu waandamanaji wa Hong Kong, anaonyesha kuwa taasisi yake ni chombo kingine cha Marekaniu kuingilia katika masuala ya eneo maalum la kiutawala," yanasema maoni yaliyoandikwa katika gazeti la kila siku linalomilikiwa na serikali.

Maoni katika gazeti jingine la Global Times lenye mrengo wa kizalendo lilisema "sasa kuna nafasi ndogo ya muafaka" kwa kuwa suala hilo limekua hadi kuingilia masuala ya maadili ya China na Marekani.

NBA imejenga wigo mkubwa wa mashabiki katika soko lenye fedha la China, juhudi zikiwa zimetiwa nguvu na umaarufu wa mchezaji wa zamani wa klabu ya Rockets, Yao Ming.

Lakini baada ya ujumbe huo wa Twitter wa Morey, kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali cha CCTV na kampuni ya internet ya Tencent zote zilizuia matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Rockets na mechi mbili za kujiandaa kw amsimu za NBA nchini China.

Chama cha Mpira wa Kikapu cha China, ambacho sasa kinaongozwa na Yao, pia kimevunja mahusiano na Rockets.

Mzozo huo umekuwa zaidi leo Jumatano wakati Silver akiwa amejiandaa kwenda Shanghai kuona mechi baina ya LA Lakers na Brooklyn Nets.

Shirikisho la Michezo la Shanghai lilifuta mpango wa tamasha la mashabiki la leo usiku kwa ajili ya kutangaza mechi ya Lakers-Nets game, iliyopangwa kufanyika siku inayofuata.

Lilisema sababu za kufuta tukio hilo ni Morey kutoa "kauli ambayo si sahihi" na Silver kuonyesha "msimamo ambao si sahihi".

Ubashiri umekua nchini Marekani kwamba hata mechi, ambazo mojawapo itachezwa katika mji ulio kusini wa Shenzhen, zitafutwa pia.

Hong Kong imekuwa katika maandamano ya karibu miezi minne, mzozo ambao uliibuka baada ya kuwepo mipango ya kuwasilisha muswada wa kuwahamishia China watuhumiwa wa uhalifu kutoka katika visiwa hivyo.

Mzozo huo uligeuka kuwa wa kudai demokrasia zaidi na kuwajibika kwa polisi, huo ukiwa mzozo mkubwa katika uongozi wa China wa visiwa hivyo tangu ikabidhiwa na wakoloni wa Uingereza mwaka 1997.

Serikali ya China imekuwa ikionya mara kwa mara kampuni za kigeni dhidi ya kuzungumza au kufanya vitendo vyovyote vya kuunga mkono waandamanaji, ikizikumbusha kuwa zinaweza kunyimwa fursa ya soko la watu bilioni 1.4.

Kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple, ambayo ina wigo mpana nchini China, imegeuka kuwa moja ya kampuni zinazowindwa.

Katika safu ya maoni ya gazeti la People's Daily, ambalo linamilikiwa na chama tawala cha CPC, lilishutumu programu ya usafiri iliyopo stoo ya Apple ikidai kuwa inawasaidia waandamanaji kutambua polisi katika visiwa vya Hong Kong. 

"Kuruhusiwa kwa programu ya Apple kunasaidia waandamanaji," ilisema habari hiyo. "Hii inamaanisha kuwa Apple ilitaa kusaidia waandamanaji?"

Baadaye habari hiyo inaonya: "Programu ya ramani ni kitu kidogo tu katika suala kubwa", ikituhumu kuwa wimbo unaotumiwa kuunga mkono uhuru wa Hong Kong upo pia kwenye stoo ya muziki ya Apple.

"Hakuna mtu anayetaka kuiingiza kwa nguvu Apple katika mzozo wa Hong Kong. Lakini watu wana sababu ya kuhisi kuwa Apple inachanganya biashara na siasa na hata vitendo visivyo halali kisheria," ilisema habari hiyo.