NCCR-Mageuzi kusimamisha wagombea ngazi zote uchaguzi mkuu 2020

Thursday February 13 2020

NCCR-Mageuzi kusimamisha wagombea ngazi zote uchaguzi mkuu 2020,Mwenyekiti wa  NCCR-Mageuzi, James Mbatia,CHAMA ,SIASA,UCHAGUZI,

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa  NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema chama hicho cha upinzani nchini Tanzania kitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.

Mbatia ambaye pia mbunge wa Vunjo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2020 katika mkutano wa waandishi wa habari kuhusu namna chama hicho kilivyojipanga kushiriki uchaguzi huo.

Amesema wataweka wagombea wa udiwani, ubunge na urais kwa maelezo kuwa chama hicho ndio kimeasisi mageuzi nchini.

Amesema lengo la chama chochote cha siasa ni kupata mamlaka kupitia vyombo vya uamuzi ili kuwatumikia Watanzania.

“Jana tulifanya kikao tumeamua kushiriki kwenye uchaguzi huu. Tutashiriki ngazi ya urais Tanznaia Bara na Zanzibar, na pia ubunge, uwakilishi na udiwani,” amesema Mbatia.

Kwa mujibu wa Mbatia,  Februari 19, 2020 watafanya  kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho kuweka mikakati ya pamoja na kutoa ratiba ya chama ya namna mchakato huo utakavyokuwa .

Advertisement

Kuhusu ushirikiano na vyama vingine vya upinzani Mbatia amesema, “hili suala kubwa kidogo linalohusu katiba yetu ya chama  na chombo kikubwa na uamuzi ni halmashauri kuu ya NCCR-Mageuzi. Baada ya kikao tutatoa maazimio yetu kuhusu jambo hili.”

 

Advertisement