NEC yatoa ufafanuzi Lissu kuzuiwa kufanya kampeni Kilwa

Muktasari:

Polisi jana Ijumaa Oktoba 23, 2020 walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuzuia mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu mjini Somanga, Kilwa kwa maelezo kuwa mkutano huo haukuwa halali.

Dar es Salaam.  Polisi jana Ijumaa Oktoba 23, 2020 walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuzuia mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu mjini Somanga, Kilwa kwa maelezo kuwa mkutano huo haukuwa halali.

Lissu alikuwa katikati ya mkutano wake wakati polisi walipofika na kumtaka aondoke eneo hilo licha ya madai yake kwamba alikuwa kihalali.

Lissu katika utetezi wake amedai alikuwa ameandika barua kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuomba kibali cha kuruhusiwa kufanya kampeni Somanga kwa sababu hakukuwa na mgombea mwingine aliyepangwa kufanya kampeni.

NEC wamekiri kupokea barua kutoka kwa Lissu akitaka kufanya mkutano wa kampeni huko Somanga.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Charles Mahera amesema kufuatia barua hiyo, ilitakiwa kuwe na mkutano na vyama vingine vya kisiasa kukubaliana juu ya mabadiliko ya ratiba.

Kulingana na ratiba ya NEC, Lissu alitakiwa kufanya kampeni Lindi, Nachigwea na Mtwara.

 “Kabla mkutano haujapangiwa kuamua juu ya mabadiliko Lissu aliamua kufanya kampeni huko Somanga. Lakini ninachoweza kusema ni kwamba, tulikuwa bado tumeketi kuamua juu ya upangaji wa ratiba, ”alisisitiza.

Baada ya mkutano wake kutawanywa, Lissu alielezea kwamba helkopta yake iliruhusiwa kutua Kilwa kwa sababu alikuwa na ruhusa ya kufanya hivyo.

 "Nimekuja hapa kwa amani kufanya mkutano wangu lakini kuna watu ambao wanataka kusababisha machafuko waache waendelee na dhamira yao, tutafanya kile tumekuja kufanya kwa amani" alisema.

Alibainisha kuwa mamlaka pekee inayoshughulika na ratiba ya kampeni ilikuwa NEC na sio vyombo vingine vya dola.

 

Wakati huo huo akiwa Lindi, Lissu alikiri kwamba ana tiketi ya ndege kwenda Ulaya Desemba 18 mwaka huu ambapo anatarajia kwenda kupata matibabu zaidi.

 "Ni kweli kwamba nina tiketi, nina miadi na daktari wangu kukagua mguu na mkono wangu ambao bado ninapata matibabu," alisema.

 Alisisitiza kuwa ikiwa angetaka kukaa mbali na Tanzania, angeweza kufanya hivyo baada ya kupigwa na risasi Septemba 16, 2017.