NMB yazindua huduma ya Masta Boda kuwawezesha madereva bodaboda

Wednesday October 16 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama akiwa amepozi kwenye bodaboda kama abiria kuashiria kuzinduliwa kwa mfumo wa malipo unaowezesha abiria wa vyombo hivyo kulipa nauli kwa kutumia simu na fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya NMB ya dereva husika. 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu nchini Tanzania, Jenista Mhagama amewataka waendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ kuwa na nidhamu ya fedha sambamba na utamaduni wa kuzitunza bila kujali kiasi gani wanachopata kwa siku.

Amesema sekta hiyo kwa sasa inatambulika na kuheshimika, wahusika nao hawana budi kuonyesha kuwa wana mchango kwenye pato na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Waziri Jenista anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 16, 2019 alipokuwa akizindua huduma ya Masta Boda, mfumo unaowawezesha abiria na wateja wake kulipa nauli kwa kutumia simu za mkononi na fedha hizo kwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya NMB ya dereva husika.

Amesema Serikali inatambua uwapo wa kundi kubwa la vijana linalojishughulisha na shughuli hiyo halali akieleza kuwa ni wakati sasa kwao kujiunganisha na taasisi nyingine rasmi kama benki.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa benki na taasisi za kifedha pamoja na kuchukua hatua pale zitakapoonekana changamoto zinazokabili teknolojia mpya zinazowawezesha vijana kujiajiri.

“Kuwa na fedha ni jambo moja ila namna ya kuzitumia ni jambo lingine, kuna haja ya mafunzo kutolewa kwenu yatakayowaongoza katika matumizi mazuri ya fedha kwa ajili ya maendeleo ya sasa na baadae.”

Advertisement

“Nimeambiwa kwa sasa hamtapata shida, abiria anaweza kukulipa kutoka katika benki yoyote na ikaingia kwenye akaunti yako,” amesema waziri huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema huduma hiyo inatoa fursa kwa maelfu ya madereva wa bodaboda nchini kutumia huduma za benki, hatua itakayoimarisha usalama wa fedha na wao wenyewe.

“Hii ni namna bora ya kurudisha uwajibikaji kwa shughuli za madereva bodaboda ambao mchango wao kwenye uchumi wa Taifa unatambulika. Tunazindua huduma hii Jijini Dar es Salaam kisha tutaenda Mwanza, Arusha, Ruvuma, Dodoma na Mbeya wiki chache zijazo,” amesema.

Ruth amesema mfumo huo wa malipo utawasaidia pia madereva bodaboda kukuza biashara zao kwa kuwapunguzia adha ya kuhifadhi fedha taslimu na kuwapa fursa ya kuepuka matumizi yasiyokuwa na mpangilio.

“Kwa kutumia MasterCard QR, tunatoa huduma ya uhakika wa malipo kwa madereva bodaboda kutoka kwa watoa huduma wote na benki za biashara wanaotumia huduma hii.  Malipo yatafanywa kwa kutumia simu ya mkononi yenye programu ya MasterCard QR na kupunguza hatari za kumiliki fedha taslimu,” amesema Ruth.


Advertisement