Naibu Spika Tulia awahamasisha wanawake kugombea nafasi za juu za uongozi

Muktasari:

Tulia amefafanua kwamba wasichana na wanawake wengi nchini wanakosa nafasi za kushiriki kwenye chaguzi kwa sababu hawajiamini na kushikilia dhana potofu kwamba nyadhifa za uongozi ni za wanaume pekee.

Dar es Salaam. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amewataka wasichana na wanawake nchini kujiamini na kujikubali kama wanataka kushikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi.

Tulia amefafanua kwamba, wengi wao  wanashindwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi kwa sababu hawajiamini na kuamini nyadhifa za uongozi ni za wanaume pekee.

 “Rais alinichagua kuwa Mbunge kwa sababu alifahamu nina uwezo wa kutosha kuwa kiongozi. Kwa hiyo, nawasihi wasichana na wanawake mtimize ndoto zenu,” amesema Tulia.

Naibu Spika huyo ameyasema hayo jana Oktoba 9, 2019 kwenye kongamano la Sauti za Wasichana lililoandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF).

“Tanzania ni nchi ya pili baada ya Rwanda na ya 28 barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya washiriki wanawake bungeni.”

 Chini ya ufadhiri wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uswidi (Sida), CDF iliandaa kongamano kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswidi na Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kuelekea maadhimisho wa siku ya mtoto wa kike duniani ambayo kilele chake ni kesho Ijumaa Oktoba 11.

 Kongamano hilo lilijumuisha wasichana na wanawake zaidi ya 170 wenye umri kuanzia miaka 15 - 25 kutoka Dar es Salaam, Dodoma na Mara, kujadili mada mbalimbali zikiwemo; wanawake na uongozi, mifumo ya kisheria na kisera, mila kandamizi, ukatili wa kingono na afya ya uzazi.

 Kwa upande mwingine, Tulia amewataka wasichana na wanawake nchini kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Tanzania Bara, chaguzi zinatarajiwa kufanyika katika vijiji 12,319 kulingana na taarifa ya Tamisemi.

Tulia pia ameeleza kwamba Serikali imeshatia saini mikataba ya Kitaifa na Kimataifa inayohusiana na usawa wa kijinsia na pia kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana na wanawake.

 Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Lennyster Byalugaba amesema lengo la kongamano hilo ni kuwapa motisha na kuwajengea uwezo wasichana na wanawake.

 Pia alimuomba Naibu Spika Tulia kuendelea kuhamasisha ajenda ya kuwasaidia wasichana na wanawake nchini akiwa kwenye vikao vya Bunge. 

“Naipongeza Serikali kwa kuanzisha Sera ya Elimu Bure, wasichana na wanawake wengi wamepata fursa ya kusoma,” amesema Lennyster.

Miongoni mwa washikiri wakati wa Kongamano, alikuwepo pia Balozi wa Uswidi nchini Tanzania Anders Sjöberg ambae aliahidi kwamba Ubalozi utaendelea kushirikiana na CDF na Serikali katika kuwawezesha wasichana na wanawake Tanzania.