Nape asema uendeshaji wa siasa unatokana na ilani ya CCM

Muktasari:

  • Mbunge wa Mtama nchini Tanzania (CCM), Nape Nnauye amesema mabadiliko ya uendeshaji siasa nchini yanatokana na kazi iliyofanywa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM huku akimpongeza, Rais John Magufuli kwa utekelezaji huo.

Dodoma. Mbunge wa Mtama nchini Tanzania (CCM), Nape Nnauye amesema mabadiliko ya namna ya kuendesha siasa nchini yametokana na kazi iliyofanywa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).
Akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/21 bungeni leo Aprili 6 mwaka 2021, Nnauye amemsifu Rais John Magufuli amefanya kazi kubwa kwenye utekelezaji wa Ilani hiyo.
Ameomba Watanzania wampe nafasi tena ya kuongoza miaka mitano ijayo kwa kuwa anatosha.
Amefanya mabadiliko na kuondoa utamaduni uliojengeka ikiwemo wa uendeshaji wa siasa.
“Ukienda siasa wasilishazoea hivyo hivyo, kuna kelele ndio lakini ukiangalia namna tunavyofanya tumekuwa more serious ukiangalia watani zangu Chadema wamefanya uchaguzi, wamefanya ACT angalia walivyofanya, kuna mabadiliko kwenye uendeshaji wa shughuli zetu,”amesema.
Mbunge huyo amesema kuwa anaamini mabadiliko hayo ni kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na kwamba Rais Magufuli na Serikali yake.
“Wamefanya kazi vizuri kwa kuitendea haki Ilani ya uchaguzi hata mtaani watu wamebadilika wapo sasa serious,”amesema.
Nape alisema yeye kama katibu mwenezi mstaafu ambaye alisimamia utengenezaji wa ilani hiyo kazi nzuri imefanyika.
“Kazi ya kubadilisha utamaduni wa namna tunavyofanya mambo kwenye nchi yetu. Tuliweka slogan ya hapa kazi tu ilitokana na utamaduni watu waliokuwa wamejijengea, kupata kipato kikubwa hakilingani na kazi inayofanyika, kwenye uchumi vyuma vinakaza lakini vinakaza kwa sababu tulizoea dili, dili zikifungwa kwa vyovyote vile vyuma vinakaza,”amesema.
Hata hivyo, amesema mapungufu ya hapa na pale katika kutengeneza mambo hayo na wakakanyagana vidole yatumike vizuri kusaidia kurekebisha mambo ili Tanzania iendelee kusonga mbele.
Pamoja na hayo alishauri suala la studio ya Bunge liwekwe kikanuni ili iwe sehemu ya uendeshaji wa shughuli za Bunge.