Ndugai, Masaburi, Ritha Mlaki wajitosa uspika

Mbunge mteule wa Jimbo la Kongwa, Job Ndugai akirudisha fomu za kuwania nafasi ya uspika kwa Katibu wa Oganizesheni, Mohamed Seif Khatib Dar es Salaam jana. Picha na Adam Mzee wa CCM

Muktasari:

Hadi jana, waliojitokeza wamefikia 19 ambao mmoja wao atachaguliwa kushindana na wagombea wa vyama vingine kuwania nafasi hiyo wiki ijayo.

Dar es Salaam. Idadi ya makada wa CCM waliojitokeza kuwania uspika wa Bunge la Kumi na Moja imeongezeka kutoka tisa hadi 19.

Juzi, wanachama tisa wa chama hicho walijitokeza ikiwa na siku ya kwanza ya uchukuaji na jana wakaongezeka wengine 10, wengi wao wakiwa kwenye kundi la waombaji ambao si wabunge.

Waliojitokeza jana ni aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 10, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Ackson, aliyekuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi pamoja na Ritha Mlaki aliyewahi kuwa naibu waziri wizara za ardhi, nyumba, makazi na viwanda na biashara.

Pia, wamo Mbunge wa Afrika Mashariki, Abdullah Ally Mwinyi, Agnes Makune, Veraikunda Urio, Julius Pawatila, Mwakalila Watson na Dk Metado Kalemani.

Wanachama hao kama ilivyokuwa kwa wenzao wa juzi, walijaza fomu hizo katika ukumbi wa mkutano na kuzirejesha kabla ya saa 10.00 jioni baada ya kulipa ada ya Sh500,000.

Hadi jana, majina makubwa yaliyokuwa yanatajwa na hayakujitokeza ni ya Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda na aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azaan Zungu.

Katibu wa NEC, Oganazesheni ya chama hicho, Dk Muhammed Seif Khatibu alithibitisha kutokuwapo kwa majina hayo miongoni mwa waliojitokeza.

Waombaji hao, wanaungana na wenzao waliojitokeza juzi ambao aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, Dk Emmanuel Nchimbi, Balozi Philip Marmo, Dk Kalokola Muzzamili, Simon Rubungu, Leonce Mulenda, Gosbert Blandes, George Nangale na Banda Sonoko.

Wagombea wajinadi

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Ndugai alisema sababu za kugombea nafasi hiyo ni kutaka kutumia uzoefu na uwezo alionao katika uongozi ndani ya Bunge.

Alisema hawezi kujua washindani wake lakini kwa kutumia Bunge hilo kama naibu spika kwa miaka mitano na kufanya kazi za Bunge akiwa na Sitta na baadaye Makinda ni vigezo pekee vinavyohitajika kwa uongozi wa chombo hicho.

“Bunge la Kumi na Moja litakuwa na changamoto zake ikiwamo wingi wa wabunge vijana na wa upinzani, kwa hiyo unahitajika uzoefu, litakuwa tofauti sana na mabunge yaliyopita,” alisema.

Ndugai ambaye pia ni mbunge mteule wa Kongwa, alisema endapo atapewa nafasi hiyo atahakikisha Bunge linaisimamia ipasavyo Serikali ili kuendana na kasi ya Rais John Magufuli.

Dk Masaburi alitaja mambo matatu yaliyomsukuma ambayo ni uwezo, uzoefu katika uongozi na kiwango cha elimu yake.

Alisema anajivuania taaluma katika mikataba, ununuzi wa umma, uhasibu na uzoefu katika uongozi wa nafasi ya umeya.