Ndugai, Ole Medeye kuchuana uspika

Mbunge mteule wa Kongwa, Job Ndugai

Muktasari:

Ndugai alipitishwa jana katika kikao cha wabunge hao, baada ya washindani wake, Dk Tulia Ackson na Mbunge wa Afrika Mashariki, Abdulla Mwinyi kujitoa.

Dodoma. Kamati ya wabunge wa CCM imempitisha kwa kauli moja mbunge mteule wa Kongwa, Job Ndugai kugombea uspika wa Bunge kwenye uchaguzi unaofanyika leo.

Kwa uteuzi huo, Ndugai ambaye alikuwa naibu spika katika Bunge la 10, atachuana na wagombea wengine kutoka vyama vinane vya siasa, akiwamo naibu waziri wa zamani wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Goodluck ole Medeye kutoka Chadema akiungwa na vyama vinavyounda Ukawa vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Ndugai alipitishwa jana katika kikao cha wabunge hao, baada ya washindani wake, Dk Tulia Ackson na Mbunge wa Afrika Mashariki, Abdulla Mwinyi kujitoa.

Saa chache kabla ya Dk Ackson kujitoa, naibu huyo wa mwanasheria mkuu wa Serikali aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge, hatua ambayo wadadisi wa mambo ya kisiasa walisema ni kuandaliwa kuwania nafasi ya naibu spika, ambayo kwa mujibu wa Katiba anayechaguliwa lazima awe mbunge.

Taarifa zilizopatikana baadaye jioni zilithibitisha Dk Ackson kuchukua fomu ya kuwania unaibu spika, akipambana na Magdalena Sakaya kutoka CUF ikiungwa mkono na Chadema pamoja na NCCR-Mageuzi.

Uteuzi wa Dk Ackson

Mapema jana, Rais Magufuli alimteua Dk Ackson kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na anatarajiwa kuapishwa katika mkutano wa kwanza wa Bunge la Kumi na Moja unaoanza leo mjini Dodoma.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 66(1)(e) ambayo inampa madaraka Rais kuteua wabunge wasiozidi 10. Baadhi ya wabunge wa CCM waliozungumza na Mwananchi kwa masharti ya kutokutajwa gazetini walisema tayari chama hicho kimeshapitisha msimamo wa Dk Ackson kuwania unaibu spika.

Kauli ya Nape

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jina la Ndugai lililopitishwa na wabunge wa CCM litapelekwa bungeni kupigiwa kura na wabunge wote.

“Tunaamini kuwa Ndugai ni chaguo sahihi bila shaka hakuna mgombea atakayemshinda na wabunge wote wa CCM wamejiridhisha,” alisema.

Alisema wagombea wengine wawili walijitoa kwa sababu wanaamini Ndugai anaiweza nafasi hiyo.

Ahadi ya Ndugai

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupitishwa na CCM, Ndugai alisema Bunge la Kumi na Moja litakuwa la demokrasia kubwa na litafanya kazi yake ya kuisimamia na kuishauri Serikali kwa ubora akiahidi kutenda haki kwa wabunge wa vyama vyote vyenye uwakilishi ndani ya Bunge hilo.

“Naomba wabunge wote waniunge mkono kwa kunipa kura nyingi katika uchaguzi na nitawatendea haki wote bila kujali vyama vyao,” alisema.

Wagombea wengine

Mbali na Ndugai na Ole Medeye, wagombea wengine sita waliiomba kuwania nafasi hiyo katika vyama vyao na kisha majina yao kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge ni Hashim Rungwe (Chaumma) na Richard Lyimo (TLP), Godfrey Malisa (CCK), Peter Sarungi (AFP), Hassan Almasi (NRA) na Alexander Kisimini (DP).

Mgongano wa kikatiba

Katika hatua nyingine, wanasheria wameonya kuwa Tanzania itaingia katika mgogoro wa kikatiba endapo Bunge la Muungano litaendelea na vikao vyake bila kuwapo uwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanasheria hao wakiwamo mawakili wa Mahakama Kuu, walidai kuendelea kuchagua Spika na naibu wake leo bila uwakilishi wa Zanzibar ni kuvunja Katiba. Kukosekana kwa wawakilishi hao kunatokana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi Oktoba 28 akisema haukuwa huru na wa haki kutokana na dosari mbalimbali lakini akasema uchaguzi wa Rais wa Jamhuri na wabunge visiwani humo ulikuwa halali.

Wanasheria hao wameegemea Ibara ya 66(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake, inayoweka muundo wa Bunge unaotambua wajumbe hao.

Ibara hiyo imeainisha aina ya wajumbe watakaounda Bunge la Jamhuri kuwa ni wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi, wabunge wa kuteuliwa na wawakilishi wa BWZ.

Kwa mujibu wa Ibara ndogo ya 1(c) ni takwa la kikatiba la kuwapo wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake, wawili wakiwa wanawake.

Wakili wa kujitegemea, Albert Msando alisema suala la wabunge watano kutoka Zanzibar siyo la akidi, bali muundo lililowekwa kwa mujibu wa Katiba.

“Katiba haikutungwa kuweka wabunge hao ili kufikisha quorum (akidi). Ni wazi kabisa wabunge hao wapo kuiwakilisha Zanzibar kama mdau wa Muungano... Hata kama akidi ipo lakini uwakilishi wa Zanzibar haupo. Hii ni dharau kwa mdau wa Muungano. Zanzibar itakuwa haijashiriki kumchagua Spika, naibu Spika wala kumpitisha waziri mkuu... Hizi ni nafasi nyeti ambazo pande zote za Muungano lazima zishiriki.”

Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS), Tawi la Moshi, David Shilatu alisema: “Kutokuwapo kwa watu hao tunavunja Katiba. Tulitakiwa tutatue kwanza huo mgongano wa Katiba na yote haya yanatokana na kuwa na Katiba yenye mgongano mkubwa.” Wakili mwingine wa kujitegemea, Elikunda Kipoko, alisema bahati mbaya watu wanaohoji kuhusu mgogoro huo hoja zao zinapanguliwa kwa hoja nyepesi ya uwepo wa wabunge kutoka Zanzibar.

“Tuna mgogoro mkubwa wa kikatiba. Bila kuwapo kwa wawakilishi hao watano, Bunge halijakamilika. Mnakwendaje kufanya uamuzi mzito kama kuchagua Spika hao wawakilishi hawapo?” alihoji.

Nyongeza na Daniel Mjema