Ndugai adai utoro wa Mbowe bungeni unawanyima fursa wapinzani

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakosa nafasi za mara kwa mara kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu kwa sababu ya utoro wa kiongozi wake, Freeman Mbowe.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakosa nafasi za mara kwa mara kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu kwa sababu ya utoro wa kiongozi wake, Freeman Mbowe.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 14, 2019 bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Amesema katika kipindi hicho swali la kwanza huulizwa na kiongozi wa kambi hiyo.

“Ndio utaratibu wetu, ndio  fursa pekee. Kwa hiyo kiongozi wa upinzani asipokuwepo bungeni siku nyingine, anapaswa kuwepo Alhamisi siku ya maswali kwa waziri mkuu.”

“Hatujapata swali hilo kwa sababu kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni hayupo. Hata uwe wapi kama spika hana taarifa zako wewe ni mtoro tu. Ndio maana mnaona leo fursa ambayo imewekwa kikanuni haijatumika,” amesema Ndugai.

Amesisitiza kuwa mara kwa mara fursa hiyo inapotea kwa sababu ya utoro.