Ndugai akomalia msimamo wake mawaziri watoro

Muktasari:

  • Pamoja na mawaziri waliotajwa kuwa watoro, kutetewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Jenista Mhagama aliyedai kuwa mawaziri hao wana kibali cha ofisi ya Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesisitiza kuwa mawaziri na wabunge hao wanapaswa kujirekebisha.

     

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameendelea kusisitiza kuwa mawaziri na wabunge aliowatangaza kwa utoro bungeni wanapaswa kujirekebisha na kuhudhuria vikao hivyo kama walivyoomba kwa wananchi wa majimbo yao kuwawakilisha bungeni.

Kauli ya Spika Ndugai imekuja baada ya Novemba 15 kuwatangaza bungeni mawaziri watano na wabunge 10 kuwa wanaoongoza kwa utoro, huku Serikali ‘ikiwatetea’ mawaziri wake kwamba ina taarifa zao pindi wanapokuwa nje ya Bunge.

Novemba 16, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Jenista Mhagama akiwazungumzia mawaziri hao wanaodaiwa na Ndugai kuwa ni watoro, alisema wote wanaokuwa nje ya Bunge huwa wanapata kibali kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.

“Sisi ndani ya Serikali tuna utaratibu, waziri anapotoka bungeni lazima apate kibali kwake au ofisi yake, hakuna waziri anayeondoka bila kupata kibali,” alisema Mhagama.

Hata hivyo, Ndugai juzi alizungumza na Mwananchi lililotaka kujua kama alipowatangaza mawaziri hao bungeni alikuwa amewasiliana na Serikali.

“Tunawasiliana na Waziri (Mhagama). Iko hivi, tamko hili ni la siku 100 za kazi, mtu anahudhuria siku saba yaani kila siku huji. Hapo kuna maelezo hapo, hata kama unaomba ruhusa utakuwa unaomba ruhusa kila siku, yaani unahudhuria siku 10 kati ya 100.

“Hivi hata hapo gazeti la Mwananchi unaweza kuomba ruhusa katika siku 100 za kazi unahudhuria siku 10 na hazijaongozana. Hivi tangu Aprili hadi Novemba na waziri anashindwa kuhudhuria vikao ambavyo si vya mfululizo, huo mfano tu halafu unasema unaomba ruhusa?

“Ni kweli kuna wakati wanashughulikia mambo ya kitaifa, lakini lazima ‘kubalance’ kidogo maana baadhi ya mawaziri ambao tunawapenda sana ni wabunge na waliomba kuwakilisha wananchi bungeni,” alisema Ndugai.

Alisema mawaziri hao wanatakiwa wawepo bungeni ili kupokea matatizo ya wananchi yanayotolewa na wabunge bungeni.

Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, alisema kauli yake haikulenga kumlaumu mtu bali kukumbushana.

Kuhusu ufafanuzi wa Waziri Mhagama na Spika Ndugai, Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare alisema dosari ya mawasiliano iliyojitokeza katika mihimili hiyo ni aibu na inatakiwa kukemewa.

Profesa Mohammed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema hatua hiyo ya kutaja majina ni uamuzi mzuri unaoweza kuongeza uwajibikaji na mahudhurio kwa wabunge na mawaziri.

“CCM ina wabunge wake na bahati nzuri Spika pia ni mbunge wa CCM kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa Katibu Mkuu wa CCM (Dk Bashiru Ali) kuwasiliana na Spika ili kutekeleza agizo lake, itasaidia kurejesha nidhamu kwa sababu wako wabunge wafanyabiashara wanaweza kupuuza baadhi ya vikao ili wafanye shughuli zao,”alisema Profesa Bakari.

Suala la utoro bungeni hasa kwa wabunge wa CCM liliwahi kuzungumzwa Juni na mwenyekiti wa CCM, Magufuli aliyemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuwaandikia barua wabunge wote wasiohudhuria vikao vya Bunge wakati wa upigaji kura za kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19.

Rais Magufuli alimtaja waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa hakuhudhuria kikao hicho kwa kuwa alikuwa amelazwa, lakini akipokea barua kutoka kwa Dk Bashiru atapaswa kuambatanisha na vyeti vya hospitali.

Mawaziri waliotajwa na Spika Ndugai kwa utoro na asilimia zao kwenye mabano ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (45) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (41).

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (38); Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba (37) na Waziri wa Mambo ya Mambo Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga aliyepata asilimia tano.

Upande wa wabunge walio katika mahudhurio ya chini wakiongozwa na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyepata asilimia 7.8 ni Salim Hamis Salim (Meatu-CCM); Mansour Yusuph Himid (Kwimba-CCM); Abdul Azizi (Morogoro-CCM); Hussein Nassoro Amar (Nyangwale-CCM); Mbaraka Bawazir (Kilosa-CCM); Dk Mathayo David (Same Magharibi-CCM).