Ndugai atoa mchanganuo idadi ya wabunge bungeni

Muktasari:

Spika Job Ndugai ametoa mchanganuo wa wabunge waliopo bungeni hadi leo Ijumaa Novemba 13, 2020 akieleza kuwa wanasubiriwa wabunge 33  ili kukamilisha idadi kamili ya wabunge wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema wamebaki wabunge 33 ili kukamilisha Idadi kamili ya wabunge wanaotakiwa kuwepo katika Bunge la 12 linalozinduliwa leo Ijumaa Novemba 13, 2020 na Rais John Magufuli.

Amesema wanaosubiriwa ni watano kutoka Baraza la Wawakilishi (BLW), wanne kutoka chama cha ACT-Wazalendo, 10 wa kuteuliwa na Rais na 19 wa Viti Maalum kutoka chama cha Chadema.

Ndugai ameeleza hayo leo muda mfupi kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli kutoa hotuba ya kulifungua Bunge.

Ndugai amesema kikatiba Bunge hilo linapaswa kuwa na wabunge 393 lakini waliopo hadi leo ni 359, “bado wanasubiriwa wabunge watano kutoka baraza la wawakilishi na viti maalumu kutoka vyama vingine na wateule wa Rais.”

“Tunasubiri wateule wa kwako 10, wanawake watano, wanaume watano na wale wa viti maalumu kutoka vyama vingine kadri watakavyokuja.”

“Katika hao 359 waliopo sasa yupo mwanasheria mkuu wa Serikali, wabunge wa CUF watatu, tunapaswa kuwa na wabunge wa ACT- Wazalendo wanne, mbunge wa Chadema mpaka sasa hivi ni mmoja na tuna wabunge wa CCM 256,” amesema Ndugai.

Aidha ameongeza kuwa kati ya hao wabunge wa viti maalumu ni 94 wa CCM wakijumlishwa na wengine 24 wa majimbo kunafanya wabunge wanawake kuwa 118 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingine lakini pia katika wabunge hao 359 waliopo bungeni sasa wapya ni 206 sawa na asilimia 61.1.