Nyerere ang’atuka 1985, akwama kumwachia ofisi Dk Salim

Safari ya uongozi wa juu wa Mwalimu Julius Nyerere wa miaka 21 ulitimia mwaka 1985 alipong’atuka madarakani.

Baada ya kuhudumu nafasi mbalimbali na mapambano ya kudai Uhuru wa Tanganyika kupatikana Desemba 9, 1961, Nyerere alishika wadhifa wa Rais Oktoba 29 mwaka 1964 hadi Novemba 5, 1985.

Ni miaka 21 ya kuipitisha Tanganyika/Tanzania katika mapito mbalimbali ya kiuongozi na hatimaye Mwalimu Nyerere akatii matamanio yake aliyoyataka tangu mwaka 1975 ya kumwachia ofisi kiongozi mwingine.

Matamanio ya Mwalimu Nyerere yalikuwa kuona anayemwachia madaraka ni Dk Salim Ahmed Salim ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu lakini hilo halikufanikiwa badala yake, Ali Hassan Mwinyi akachukua mikoba yake.

Mwalimu Nyerere aling’atuka baada ya mwaka 1980 alipochaguliwa na mkutano mkuu maalumu wa CCM uliokutana Alhamisi ya Septemba 25, 1980, kuwa mgombea pekee wa kiti cha Rais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 26 mwaka huo, aliweka bayana huo ndiyo ungekuwa uchaguzi wake wa mwisho hata kama wangependekeza tena jina lake.

Waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Mateo Qaresi anasema Mwalimu Nyerere alikuwa amemwandaa Salim Ahmed Salimu kuwa mrithi wake lakini hilo lilishindikana na matokeo yake wajumbe wa mkutano wa halmashauri kuu walimchagua Mwinyi kuwa mgombea na hatimaye rais.

Anasema majina matatu yalijitokeza kuwania nafasi hiyo ambayo ni ya Mwinyi, Rashid Kawawa na Salim, “lakini baadaye Kawawa alijitoa na kubaki majina mawili la Mwinyi na Salim na kura zilipopigwa Mwinyi akashinda kuwa mgombea na Mwalimu Nyerere hakuwa na njia nyingine ilibidi akubali.”

Mateo anasema baada ya Mwinyi kuingia akaanza kurejesha uchumi ambao ulikuwa unayumba na kuanza kuachana kidogo kidogo na uchumi wa kijamaa ambao Mwalimu Nyerere aliuanzisha na hilo lilichagizwa na kuanzishwa kwa Azimio la Zanzibar.

Anasema Azimio la Zanzibar lilikuja kufanya mabadiliko ya Azimio la Arusha la mwaka 1967 na kutoa fursa kwa watumishi wa umma kuwa wafanyabiashara lakini sekta binafsi ikaanza kufanya kazi kwa baadhi ya maeneo ili kuchochea uchumi.

Mhadhiri mwandamizi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaver Lwaitama naye anasema Mwalimu Nyerere aliamini Dk Salim angekuwa mrithi wake na dalili hizo zilionekana tangu mwanzo lakini mwisho wake haikuwa hivyo.

Anasema baada ya Mwinyi kuingia madarakani alianza kubadili mifumo ikiwamo kuachana na uchumi wa kijamaa aliokuwa anauendesha Mwalimu Nyerere ambaye hakuridhika na kile alichokifanya Mwinyi ila hakuwa na namna.

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilipitisha jina la Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuwa mgombea wa kiti cha urais.

Uchaguzi wa wabunge

Mara baada ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa, kwamba ungefanyika Jumapili ya Oktoba 27, 1985, kampeni za uchaguzi wa wabunge katika majimbo yote ya uchaguzi zilianza rasmi Jumatatu ya Oktoba 14, 1985.

Ulifanyika uamuzi wa kubadili tarehe za kampeni kwa majimbo ya vijijini Jumanne ya Oktoba 1 na Tume ya Uchaguzi ambayo ilikutana katika Ofisi ya Spika chini ya mwenyekiti wake, Chifu Adam Sapi Mkwawa.

Awali kampeni za majimbo ya uchaguzi ya vijijini zilipangwa kuanza Jumatatu ya Oktoba 7 na zile za majimbo ya mijini zilipangwa kuanza Jumatatu ya Oktoba 14.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Elias Kazimoto, alisema mabadiliko hayo ya tarehe yalitokana na uhaba wa mafuta ya petroli ambayo yalitarajiwa kuanza kusambazwa nchini kote Oktoba 8 na 9.

Kuhusu wapiga kura waliohamia sehemu nyingine mbali na kule walikojiandikisha, Tume iliagiza kuwa Oktoba 15 ndiyo ingekuwa siku ya mwisho ya wapiga kura hao kutoa taarifa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili kuomba kibali cha kupiga kura sehemu walizohamia.

Tume ilitoa fursa ya pekee katika mazingira yasiyozuilika kwa mtu kupiga kura ya Rais nje ya mahali alipojiandikisha kwa kupata kibali cha Mkurugenzi wa Uchaguzi ili mtu au watu hao waweze kupiga kura katika sehemu walizokuwa siku ya kupiga kura.

Fursa hiyo ya kupiga kura ya Rais ilitolewa kwa watu waliokuwa katika taasisi maalumu zilizotambulika kama majeshi, vyuo na hospitali.

Tume pia ilichapisha mifano ya karatasi za kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na pia kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge wa majimbo ya uchaguzi. Karatasi za uchaguzi wa Rais zilikuwa na jina la mgombea pekee, yaani Ali Hassan Mwinyi.

Upande wa kushoto chini ya jina kulikuwa na nafasi yenye kivuli ambayo chini yake kulikuwa na neno ‘Hapana’ na kulia kulikuwa na picha ya Ali Hassan Mwinyi ambapo chini yake kulikuwa na neno ‘Ndio.’

Karatasi za kura za wabunge zilikuwa na majina na picha za wagombea katika kila jimbo. Chini ya picha kulikuwa na nafasi ya kuweka alama ya ‘V’ kwa yule aliyepiga kura.

Zanzibar maandalizi ya uchaguzi wa Rais wa visiwa hivyo ulikamilika mapema zaidi kuliko Bara. Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Idi Pandu Hassan, alisema tangu Oktoba Mosi tayari vifaa kama masanduku ya kupigia kura, mihuri na wino vilikuwa vimeshafikishwa katika makao makuu ya wilaya za Unguja na Pemba.

Udhibiti wa kampeni

Wakati maandalizi hayo yakiendelea, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Moses Nnauye aliwataka viongozi wa chama wasiwafanyie kampeni wagombea ubunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Brigedia Nnauye ambaye ndiye aliyekuwa anashughulikia masuala yote ya uchaguzi kwa upande wa CCM, Alhamisi ya Oktoba 3, 1985, aliwaita waandishi wa habari mjini Dar es Salaam na kuwaambia kuwa viongozi hawatakiwi kujiingiza katika kuwafanyia kampeni wagombea kwani wao ndiyo wasimamizi wakuu wanaoweza kutatua matatizo yanayojitokeza katika kampeni za wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kwa sababu hiyo wanatakiwa kukaa nje ya kampeni hizo.

Alisema wenyeviti na makatibu wa wilaya, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ibara ya 13, kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwa wasimamizi na wazungumzaji wakubwa katika kampeni za wagombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano na cha Urais wa Zanzibar.

Kwa Zanzibar ambako wilaya moja ilikuwa na majimbo mengi, Nnauye alisema halmashauri ya wilaya inaweza kuteua wajumbe kwenda kuzungumza kwenye kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar kwa niaba ya mwenyekiti au katibu wa wilaya.

Chama kilitoa ombi maalumu kwa wananchi wa visiwani kuhudhuria kampeni zote mbili za Serikali ya Mapinduzi za kumchagua Rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kampeni ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano. “Wananchi wa Visiwani wao wana kazi ngumu zaidi kwani wana kampeni mbili. Ninawaomba kwa niaba ya kamati kuu kuhudhuria kampeni zote mbili kwa nguvu moja,” alisema Brigedia Nnauye.

Msimamo wa Nyerere

Endapo nia ya Mwalimu Nyerere ingetimia mapema, asingefika katika uchaguzi huo kwa kuwa alikuwa ameeleza nia ya kung’atuka mapema.

Alipoteuliwa kugombea kwa mara ya mwisho mwaka 1980, alikubali lakini aliuambia mkutano huo, “nilipoteuliwa kama hivi mwaka 1975 nilisema kwa kirefu kidogo kabla sijaukubali mzigo huu. Nilisema mambo mawili.

Kwanza, nilieleza haja ya kuunganisha Tanu na ASP kuwa chama kimoja. Hilo sasa tumelifanya, na matokeo yake ni Chama cha Mapinduzi. Nchi yetu tuliyoiita nchi ya chama kimoja ingawa kwa kweli ilikuwa na vyama viwili sasa ni nchi ya chama kimoja kweli. Nadhani tuna haki ya kujipongeza kwa mafanikio hayo.”

Miaka mitano baadaye, Agosti 15, 1985 wakati wa uteuzi, Mwalimu Nyerere akiwa ni Rais na Mwenyekiti wa CCM, aliuhutubia Mkutano Mkuu Maalumu wa chama wa kumteua mgombea urais.

Akiwajibu wale waliotaka aendelee kuwa rais, Nyerere alisema: “...naelewa hoja za wale wanaonitaka niendelee ambazo kwa kweli zinaonyesha hofu ya mabadiliko katika uongozi wa juu wakati wa matatizo makubwa ya uchumi katika taifa letu. Lakini safari hii mkutano wetu utamchagua mtu mwingine. Jina jipya litapelekwa kwa wananchi kuthibitishwa.

“Hoja za kubadilisha uongozi wetu wa juu nilizozitoa mwaka 1975 bado ni za kweli mpaka sasa. Mtu mmoja anapokuwa Rais wa taifa kwa muda mrefu mno, watu huanza kuogopa mabadiliko.”

Sehemu ya hotuba hiyo inasema hivi: “Ingawa mimi mwenyewe nilieleza umuhimu wa kuleta mabadiliko hayo tangu mwaka 1975, na nikadhihirisha katika hotuba ile kwamba nisingekubali kuteuliwa tena kushika kiti cha Rais mwaka 1980, hata hivyo nilikubali jina langu kuteuliwa na kupigiwa kura na wananchi miaka mitano iliyopita.

“Nilitoa sababu mbili za kukubali kuteuliwa kwangu mwaka 1980. Kwanza—na sababu hiyo nilisema ndiyo muhimu zaidi—ni kwamba Chama wakati ule hakikuwa kimejiwekea utaratibu mzuri unaowafaa Watanzania wa kumpata mgombea mpya wa kiti cha Rais.

“Ya pili ilikuwa hali mbaya sana ya uchumi ambayo dhahiri ilikuwa inatuandama kati ya mwaka 1980 na 1985. Nilikubali uzito wa hoja kwamba kwangu mimi kukataa kuteuliwa wakati ule ingekuwa ni kama kukimbia kutoka uwanja wa mapambano ya uchumi huku vita bado inaendelea.”

Kesho tutaangazia kile kilichotokea wakati wa upigaji kura, kuapishwa kwa Mwinyi na alichokisema baada ya kuapishwa na uundaji wa baraza lake la kwanza na kile kilichojiri uchaguzi wa Zanzibar.