OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Ndege za Israel zatua Entebbe-7

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona jinsi waziri mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin alipotoa idhini kwa Jeshi la Israel kwenda kuvamia Uganda na kuwakomboa mateka wa Kiyahudi waliokuwa wakishikiliwa na magaidi katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe. Je, nini kiliendelea baada ya idhini hiyo? Endelea.

Wakati ndege zinaondoka Israel kuelekea Uganda kuokoa mateka, majasusi wa Israel walipata taarifa za kijasusi kutoka Uganda zikidai kuwa magaidi waliokuwa wakiwalinda mateka hawakuzidi kumi, lakini kulikuwa na zaidi ya wanajeshi 100 wa Jeshi la Uganda waliokuwa wamezunguka jengo walimokuwa mateka hao. Kulikuwa pia na hofu kwamba jengo hilo lilikuwa limetegewa mabomu.

Ndege ya kwanza kuondoka mjini Tel Aviv ilikuwa ni Boeing 707. Ingawa hii ilikuwa ni ndege ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), ilikuwa na rangi kama ya ndege za abiria za Shirika la Ndege la Israel (El Al) na usajili wa kawaida.

Miongoni mwa maofisa wa jeshi la Israel waliokuwa wamebebwa katika ndege hiyo ni kamanda wa Jeshi la Anga la Israel (IAF), Benny Peled. Mwingine aliyekuwa kwenye ndege hiyo pamoja na Peled ni kaimu mnadhimu mkuu wa IDF, Yekutiel Adam. Ndege hii ilifuata utaratibu na njia ya kawaida kutoka Tel Aviv kwenda Nairobi.

Ndege hii haikutiliwa shaka yoyote kwani hakukuwa na sababu yoyote kwa yeyote kufanya hivyo kwa kuwa ndege hiyo ilionekana kuwa ya kibiashara na si ya kijeshi. Lakini ndani ya ndege hiyo kulikuwa na wanajeshi na mizigo mingine ya kijeshi na ilikuwa inakwenda kwenye mapambano ya kivita.

Ndege hiyo ilitua salama mjini Nairobi na kuegeshwa eneo ambalo ndege za El Al zinaegeshwa. Ndege ilipokewa kwa ulinzi mkali wa polisi wa Kenya. Aliyekuwa kamanda wa polisi katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Lionel Davies, alikuwa ni mmoja wa maofisa wachache sana wa serikali ya Kenya waliojua kwa nini ndege hiyo ilitua uwanjani hapo na kwa nini ilipewa ulinzi mkali na kwa nini ilipelekwa moja kwa moja kwenye maegesho ya ndege za El Al.

Ndege ya pili, Boeing 707, ilifuata utaratibu wa ndege ya kwanza. Hii ndege ya pili ilikuwa na madaktari na wauguzi waliokuwa tayari kuhudumia majeruhi waliotarajiwa kutokana na pambano ambalo lingefanyika baadaye usiku huo.

Zikiwa zimeegeshwa, yalikuja magari ya kubeba mafuta na kuzijaza mafuta ndege zote mbili bila kugunduliwa. Telex ilitumwa Tel Aviv kwa bosi wa El Al, Mordecai Ben-Ari, kumjulisha kuwa ndege mbili zimetua salama.

Boeing mbili hizi zikiwa zimetulia Nairobi, ndege nne za kijeshi aina ya Hercules sasa zingeweza kuanza safari. Ziliamriwa kupaa angani saa 10 kasoro jioni kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Sharm al-Sheikh ingawa zilikuwa ni ndege za kijeshi na zilibeba wanajeshi kwenda kwenye operesheni ya kijeshi, Hercules zote nne zilibandikwa usajili wa ndege za kawaida na wakati zinaondoka Israel, marubani wake walifuata taratibu zote zinazofuatwa na ndege za abiria.

Ndege zilipoondoka na kumaliza tu anga la Israel zikashuka chini tofauti na ilivyo kawaida. Zilipokaribia Ziwa Victoria kuna wakati ndege hizo zilishuka chini zaidi kufikia futi 3,000 juu ya usawa wa bahari zikienda kwa kasi ya maili 350 kwa saa huku zikiwa zimepishana umbali wa kiasi cha kilomita moja kila moja.

Wakati ndege zikikaribia Uganda, waziri mkuu wa Israel, Shimon Peres, alikuwa ofisini kwake na mawaziri wa Israel, mmojawapo akiwa waziri wa Uchukuzi, Gad Yaakobi. Walikuwa wametegeshea vifaa vya kusikiliza kinachoendelea mjini Entebbe. Muda huo ulikuwa ni saa nne kuelekea saa tano usiku.

Hadi wakati huo mateka walikuwa wamekaa nchini Uganda kwa siku sita chini ya mtutu huku wakitishiwa kuuawa ikiwa Serikali ya Israel haitatimiza matakwa ya watekaji nyara hao.

Magaidi walikuwa wakipeana zamu kuwalinda mateka. Wakati makomandoo wa Israel wakiingia, waliokuwa zamu kuwalinda mateka ni mwanamke mmoja na mwanaume mmoja raia wa Ujerumani.

Daktari mmoja raia wa Misri alikuwa akiwahudumia baadhi ya mateka kwa sababu wengi wao sasa baadhi walikuwa wamepatwa na kipindupindu na wengine walikuwa katika hatari ya kushambuliwa na maradhi hayo.

Maji katika vyoo walivyokuwa wanatumia yalikuwa yamekatika na vyoo walivyokuwa wanavitumia vilikuwa katika hali ya uchafu. Kwa kuwa maji yalikuwa yamekatika, wanajeshi wa Uganda walileta maji lakini kwa kuchelewa.

Ndege ya kijeshi iliyotangulia ilikuwa imembeba Yonathan Netanyahu na makomandoo wengine tisa ambao walikuwa wamejibanza kwenye gari aina ya Mercedes Benz waliyotoka nayo Israel ambayo walikuwa wameipaka rangi nyeusi na kufunga bendera za Uganda. Walitaka ionekane kuwa ni gari ya Idi Amin na kwamba ndiyo kwanza amerejea kutoka kwenye mkutano wa Nchi Huru za Afrika (OAU) nchini Mauritius.

Dakika kumi kabla ndege hizo hazijaanza kutua zilipunguza mwendo hadi kufikia kasi ya maili 180 kwa saa. Waliondoka Israel katika muda uliopangwa na walikuwa wanakaribia kutua katika muda uliopangwa. Nia yao ilikuwa ni kuishambulia Entebbe wakati Waganda wakiwa usingizini na watekaji wakiwa wamepumzika bila kutarajia uvamizi wa aina yoyote. Wakati huu ndege zilikuwa zimeshaingia usawa wa Ziwa Victoria kuelekea Entebbe.

Kwa hesabu ambazo Wayahudi walikuwa wamepiga, ikiwa ndege ya kwanza ingetua Entebbe bila watekaji au wanajeshi wa Uganda kugundua, basi kazi ya kuwaokoa mateka ingekuwa rahisi, lakini kama ingegundulika kuwa ndege iliyotua ni ya wavamizi, basi usalama wa mateka na makomandoo wa Israel ungekuwa hatarini zaidi.

Hercules, ikiendeshwa na rubani wa kijeshi aliyeitwa David, ilikuwa katika hatua za mwisho kupita juu ya Ziwa Victoria kuelekea Entebbe ikifuatiwa na zile nyingine ambazo zilipishana kwa umbali wa kiasi cha kilomita moja. Kadri walivyokaribia Entebbe ndivyo marubani wote walizidi kuwa makini kuliko wakati mwingine wowote.

Makomandoo walijiweka tayari kwa lolote ambalo lingetokea. Muda ulikuwa unakwenda kwa kasi sana, na umakini wao ndio ulikuwa mwamuzi kati ya kufa au kupona. Ndege zote, baada ya kuvuka Ziwa Victoria kuingia Uganda, zilipunguza kasi hadi kufikia mwendo wa maili 20 kwa saa.

Sasa rubani David alianza kuona majengo yaliyokuwa kwenye uwanja wa zamani wa Entebbe, na miongoni mwa majengo hayo ndimo ambamo watekaji nyara walikuwa wamewashikilia mateka wa Kiyahudi. Alijitahidi sana ndege isiwe na mngurumo mkubwa wa kuwashtua wanajeshi wa Uganda waliokuwa wakiulinda uwanja huo.

Kutokana na habari za kijasusi walizokuwa wamezipokea kabla, Waisraeli walijua kiasi cha wanajeshi 21,000 waliokuwa wamepata mafunzo ya kijeshi kikamilifu, nusu yao walifikiriwa kuwa walikuwa wako katikati ya Entebbe na Kampala na kwamba Uwanja wa Ndege wa Entebbe ulikuwa unalindwa na wanajeshi waliokuwa wakitumia zana za kijeshi zilizotengenezwa Urusi vikiwamo vifaru.

Itaendelea kesho