Ofisa Nida, wakala usajili laini mikononi mwa Takukuru

Muktasari:

Mtego uliowekwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko umefanikisha kuwanasa Ofisa wa Nida na wakala wa usajili wa laini za simu kwa tuhuma za kuwatoza wananchi Sh30, 000 ili kuwapa namba za vitambulisho na kusajili laini zao za simu.

Shinyanga. Ofisa msajili msaidizi wa vitambulisho vya Taifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) mkoa wa Shinyanga, Haroun Mushi na wakala wa usajili wa moja ya kampuni za simu, Victor Vicent  wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwatoza wananchi Sh30,000 ili kuwapa namba za vitambulisho na kuwasajili.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewaambia waandishi wa habari mjini Shinyanga leo Jumatatu Januari 20, 2020 kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya mtego uliowekwa kutokana na taarifa za wananchi kuombwa fedha ili wapewe namba za vitambulisho na kusajiliwa.

“Nilipokea malalamiko hayo nilipotembelea ofisi za Nida kukagua utoaji wa namba za usajili wa laini za simu,” amesema Mboneko

Amesema baada ya kupokea malalamiko ya kuwapo wakala anayesajili laini za simu kwa alama anayeshirikiana na Ofisa wa Nida kuwatoza wananchi Sh30, 000 ili kuwapa namba na kuwasajilia laini zao, aliweka mtego na kuwanasa.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Joseph Paul amesema watuhumiwa hao tayari wamekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mahojiano na hatua zaidi za kisheria.