VIDEO: Ofisa manunuzi, mzabuni wakamatwa kwa agizo la Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda kumkamata ofisa manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Francis Muyombo kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka.

Singida. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda kumkamata ofisa manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Francis Muyombo kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka.

Pia,  amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike kumkamata Joseph Kisaka ambaye alikuwa mzabuni wa chuo hicho kwa kuwapatia vifaa vilivyo chini ya kiwango.

Ametoa maagizo hayo jana jioni Jumapili Oktoba 6, 2019 wakati akikagua ukarabati wa majengo ya chuo hicho kilichopo wilayani Iramba mkoani Singida ambako alibaini taarifa zinaonyesha kitasa kimoja kimenunuliwa kwa Sh70,000 badala ya Sh25,000. 

Majaliwa amesema taarifa ya manunuzi inaonesha walipaswa kununua vitasa ambavyo vinafunga mara tatu lakini alipokwenda kukagua milango kwenye mabweni, ukumbi, na bwalo na kukuta vitasa vya kufunga mara moja.

“Serikali imetoa Sh1.4  bilioni kwa kila chuo ili kufanya ukarabati wa vyuo vya elimu kikiwemo hiki cha kwenu. Nyinyi mnanunua vifaa kinyume na utaratibu wa Serikali, hamvikagui, mnaweka tu vitu hafifu ambavyo havidumu. Haiwezekani!”

“Inaonyesha mlinunua vitasa 368 vya 3-level kwa gharama ya Sh 70,000 kila kimoja. Lakini vitasa vilivyoko mlangoni ni vya 1-level ambavyo vinauzwa Sh25,000. Haya ni mabweni ya wanafunzi, wanaingia na kutoka kila wakati, ni kwa nini mnaweka vitu rahisi akati mnajua vitaharibika mapema? Maelekezo ya ununuzi wa Serikali yakoje,” amehoji Majaliwa.

Alipoulizwa wametumia utaratibu gani kununua vifaa hivyo, Mkuu wa Chuo hicho, Hamisi Njau amesema walikuwa wakitumia kamati ya manunuzi ambayo mwenyekiti wake alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo na Katibu wake ni ofisa manunuzi, Muyombo.

 

Muyombo alipoulizwa kama walikuwa wanayo taarifa ambayo ilikuwa ikiwaongozwa kufanya manunuzi, alijibu kwamba hawakuwa nayo bali alikuwa wakiorodhesha mahitaji yao na kuyapeleka kwa mhandisi.

Alipoambiwa aeleze tofauti ya vitasa vya 3-level na vya 1-level, Muyombo alijibu kwamba waliambiwa na mhandisi kwamba ndani ya kitasa kuna kibati ambacho kinatofautisha vitasa hivyo.

Majaliwa amesema Serikali inakataa udanganyifu kwenye manunuzi na haitavumilia watumishi wasiokuwa waaminifu. “Tena hili duka la huyo Kisaka ni la nguo wala sio la vifaa vya ujenzi.”

Alimueleza mkuu wa chuo hicho alipaswa kusimamia ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati unaofanyika chuoni hapo.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Sh1,439.235,746 ili kukarabati chuo hicho kwenye maeneo ya utawala, maeneo ya kujifunzia, kumbi na mabweni ya wanachuo. Awamu ya kwanza ya fedha hizo ilitolewa Novemba, 2017 na awamu ya pili Juni 2018.

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho baada ya kufanya ukaguzi huo, Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

 “MRais alitoa Sh1.4 bilioni kwa vyuo vyote ili kukarabati na kuboresha hadhi ya vyuo hivyo vikiwemo vya Monduli, Patandi, Kinampanda, Mtwara, Songea, Nachingwea, Korogwe, Kasulu na Butimba.”

“Nimeingia kwenye maktaba yenu nimeona bado vitabu vilivyopo ni vya muda mrefu, lakini kwa upande wa ajira bado tunaendelea kuajiri kwa awamu. Julai 2019  tuliajiri walimu 4670 na sasa hivi tumepata kibali cha kuajiri walimu 16,000,” amesema Majaliwa.