VIDEO: Ole Sabaya ataka Mbowe kuzungumza yanayoihusu Hai

Ole Sabaya ataka Mbowe kuzungumza yanayoihusu Hai

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema hawezi kumruhusu mbunge wa Hai na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuzungumzia mambo yanayohusu majimbo mengine akiwa ndani ya wilaya hiyo.


Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema hawezi kumruhusu mbunge wa Hai na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuzungumzia mambo yanayohusu majimbo mengine akiwa ndani ya wilaya hiyo.

Sabaya aliyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 katika  mahojiano na Mcl Talk, kipindi kinachorushwa na Mcl Digital alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) zilizopo Tabata Relini, jijini Dar es Salaam.

“Sitamruhusu Mbowe asimame jukwaani azungumzie mambo ya Muleba akiwa Hai. Azungumze mambo ya maendeleo, hiyo ndiyo ajenda yetu kubwa,” amesema Lengai.

Amesema nchini Marekani ambayo vyama vya siasa vinashindana wakati wa uchaguzi lakini baada ya mshindi kupatikana wote wanashirikiana katika kuijenga nchi yao huku siasa zikifanyika Bungeni.

“Hatuwezi kila siku kupishana majukwaani wakati tuna kazi ya kuijenga nchi,” amesema Sabaya na kubainisha kuwa kuna tofauti kati ya kumkosoa Rais John Magufuli kwa lengo la kumshauri na kukosoa kwa lengo la kumdhalilisha.

 Changamoto za Hai

Akizungumzia changamoto za wilaya yake, Sabaya alisema tatizo kubwa linaloikabili wilaya hiyo ni wananchi wake kudhani wanaweza kufanya jambo lolote bila kukemewa.