Oluoch ruksa kurejea kazini

Muktasari:

Katibu mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amesema naibu katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluochi anaweza kurejea kazini.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amesema naibu katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluochi anaweza kurejea kazini.

Ameeleza hayo jana Jumanne Februari 11, 2020 baada ya kuulizwa na Mwananchi  kuhusu Mahakama ya Rufani kutengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyoridhia uamuzi wa katibu mkuu Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), kumuondoa kazini Oluochi.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza rufaa hiyo ambao ni Jaji Sivangilwa Mwangesi aliyekuwa kiongozi, akishirikiana na Mwanaisha Kwariko na Rehema Kerefu baada ya kukubaliana na sababu za rufaa za Oluoch.

Katika hukumu yake, Mahakama ya Rufani imesema baada ya kusikiliza na kujadili hoja za pande zote na kurejea sheria na kanuni za utumishi wa umma, imeona katibu mkuu wa utumishi hana mamlaka ya kumuondoa mtumishi kazini.

“Kutokana na hoja hizo hapo juu ni mtazamo wetu kwamba katibu mkuu wa Utumishi alivuka mamlaka yake kwa kuwa hana mamlaka ya kutoa amri ya kumuondoa mtumishi wa umma katika utumishi,” inaeleza hukumu hiyo,

“Iko wazi kwamba kumuondoa au kuagiza kuondolewa kwa mwalimu katika utumishi si miongoni mwa mamlaka ya kisheria ya mrufani wa kwanza (katibu mkuu wa utumishi).”

Hata hivyo, imesema mwalimu anaweza kuondolewa katika utumishi na Rais kama inavyoelezwa katika kanuni ya 29 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma.

Mahakama hiyo imesisitiza kuwa ni kupitia mamlaka ya uteuzi tu ambapo Rais anaweza kuhusishwa katika kumuondoa mwalimu katika utumishi wa umma kwa maslahi ya umma.

Katika maelezo yake ya jana Dk Ndumbaro amesema amepokea  barua ya Oluoch kuhusu kesi hiyo na kutaka kurejeshwa kazini ambazo zimejibiwa, “Barua tumeshaandika kama iko njiani ama posta, basi ataipata tu. Kama ameipata ataeleza mwenyewe lakini si sawa kusema tumejibu nini. Tunawasiliana kwa njia ya posta kwa hiyo nadhani itakuwa njiani.”

Alipoulizwa endapo mtumishi huyo anaweza kurejea tena kazini, Dk Ndumbaro amesema bila shaka atarejea kazini.

Olouch pia amewasilisha barua Baraza la Taifa la CWT Januari 31, 2020 ikiwa ni wiki tatu baada ya kuwasilisha barua ofisi za utumishi.

“Muda wa uongozi bado haujaisha ndani ya CWT kwa hiyo napaswa kurejea katika nafasi yangu,” amesema Olouch.

Oluoch alifungua shauri la maombi Masjala Kuu akiiomba ifanye mapitio na kisha kutengua uamuzi wa kutimuliwa.

Katika uamuzi wake wa Aprili 18, 2018 uliotolewa na Jaji Pellagia Khaday, Mahakama ilitupa shauri lake na kuamuru aondolewe katika utumishi, ikisema kuwa hayana mashiko, ndipo akakata rufaa hiyo akipinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Alikata rufaa Mahakama ya Rufani dhidi ya katibu mkuu wa utumishi, katibu mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, katibu mkuu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), katibu wa Tume ya Walimu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika rufaa yake, Oluoch pia aliiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia katibu mkuu wa utumisha kumlazimisha kuamua suala la maombi yake ya likizo isiyo na malipo, akisema yana msingi.

Pia alikuwa akiiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio dhidi ya katibu mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, katibu mkuu wa Tamisemi, na katibu wa Tume ya Walimu kuondoa jina lake katika rejista ya watumishi wa umma chini ya mamlaka yao.