Operesheni nyakua inavyoondoka na madereva

Muktasari:

Mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma kikosi cha usalama barabarani nchini Tanzania, Abel Swai amesema madereva wasiozingatia sheria barabarani wameendelea kunyakuliwa katika operesheni nyakua.

Dar es Salaam. Mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma kikosi cha usalama barabarani nchini Tanzania, Abel Swai amesema madereva wasiozingatia sheria barabarani wameendelea kunyakuliwa katika operesheni nyakua.

Operesheni ‘nyakua nyakua’ ilizinduliwa Mei, 2018 na Kamanda wa polisi Kikosi cha Usalama barabarani, Fortunatus Muslim aliyeeleza kuwa  madereva watakaobainika na makosa ya barabarani hawatatozwa faini badala yake watapelekwa mahabusu kisha kufikishwa mahakamani.

Swai ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.

“Tunaondoa masalia ya madereva  wasio na maono ya mbele ikiwemo kutozingatia sheria za barabarani kwa kuendesha gari ukiwa unachezea simu. Inawezekanaje dereva akagawa mawazo mara mbili kwa wakati mmoja, uchezee simu huku unaendesha gari.”

“Ndio maana ‘nyakua nyakua’ ya kimya kwa kishindo ambayo inaondoa masalia. Tunataka kuwabaini wale tuliowanyakua na kubaki mmoja, nia yetu sio kukomoa,” amesema Swai.

Akizungumzia matumizi ya barabara za waenda kwa miguu, Swai amesema, “mfano mtu akiwa Vingunguti anaweza akaona msongamano wa magari eneo la Tazara akaamua  kuchepuka kwa kuingia njia mbadala kwa mwendo mkali akijua wazi kuwa hairuhusiwi.”

“Barabara mbadala hutumiwa na waenda kwa miguu na waendesha baiskeli lakini madereva wanaotumia wanafanya makosa na ni kinyume cha sheria.”

Amesema barabara hizo si imara na ndio sababu hubandikwa vibao vinavyoonyesha uzito wa magari yanayotakiwa kupita.

“Baadhi ya madereva wamekuwa wakikaidi lakini hawaijaribu polisi bali wanaijaribu sheria. Sheria ni msumeno,” alisema Swai.