Pacha auawa, mwingine ajeruhiwa kwa risasi wakituhumiwa kwa ujangili

Muktasari:

  • Askari wa wanyamapori wanaolinda Pori la akiba la Grumeti wilayani Bunda, wanadaiwa kuwapiga risasi pacha wanaodaiwa kufanya ujangili kwenye pori hilo.

Serengeti. Ndugu wawili ambao ni pacha wamepigwa risasi na mmoja amefariki dunia na mwenzake kujeruhiwa kwa risasi na askari wa wanyamapori ndani ya pori la akiba la Grumeti wilaya ya Bunda, wakituhumiwa kwa ujangili.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mara, Daniel Shila amesema hayo leo Jumanne Oktoba 15, 2019.

Akizungumza na Mwananchi, kamanda huyo amesema tayari uchunguzi umeanza kuhusiana na tukio hilo na amemtuma kamanda wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mara kufuatilia kwa kina.

“Kwa sasa sina taarifa kamili za tukio hilo, ndiyo maana nimemtuma RCO kwenda huko, akirudi atanipa taarifa nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia kwa kina,” amesema kamanda huyo.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere, Tanu Warioba amesema jana Jumatatu Oktoba 14, 2019 Saa 5 asubuhi, walipokea mwili wa Kurwa Marwa (46) na majeruhi mmoja, Dotto Marwa (46) ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Manjimweru ambao wanadaiwa kupigwa risasi.

“Majeruhi tunampeleka kwenye chumba cha upasuaji jioni hii ili kutoa gololi za risasi ambazo amepigwa mkono wa kushoto na tumboni. Mwili wa Kurwa utafanyiwa uchunguzi lakini nao bado una risasi,” amesema.