Padri asimulia mbinu mpya ya wauza dawa za kulevya

Padri John akizungumza na  Watanzania ambao ndugu zao wanatumikia vifungo Hong Kong na China,  mtumishi huyo wa Mungu alizungumza na ndugu hao juzi jijini Dar es Salaam  na kuwaeleza mambo mbalimbali,  likiwemo la mbinu mpya zinazotumiwa na wauza dawa za kulevya.

Dar es Salaam. Kaa chonjo na raia wa Nigeria wanaojaribu kukuzoea katika mitandao ya kijamii na hata kukuahidi ajira nchini Ethiopia; hiyo ni mbinu mpya ya kuingizwa katika biashara ya dawa za kulevya.

Wanaofika Ethiopia kwa ahadi hizo, hulazimishwa kubeba dawa hizo kwa kumeza au kuweka sehemu nyingine ili kuzipeleka China na Brazil.

Hayo yameelezwa na padri wa Kanisa Katoliki na mkazi wa Guangzhou nchini China, John Wootherspon, ambaye amekuja nchini kwa ajili kueneza habari dhidi ya biashara hiyo na kuizuia isienee barani Afrika.

Alisema wengi wanaolaghai watu mitandaoni ni raia wa Nigeria.

“Wengi, hasa wanawake wanadanganywa kuwa kuna kazi yenye mshahara mnono, kisha wanaambiwa wanalipiwa nauli na hati ya kusafiria,” alisema Padri Wootherspon.

“Lakini wakifika huko wanalazimishwa kumeza dawa na wakikataa hutishiwa maisha au kutishiwa kuwa familia zao zitadhuriwa.”

Alisema kwa sasa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanatumia mpaka wa Ethiopia kwa sababu hauna ulinzi makini na ni rahisi kwa wao kupenya na kuzifikisha China na Guangzhou.

Padri Wootherspon alisema kilichomfanya aje nchini mwaka huu ni kutokana na matukio ya kukamatwa kwa Watanzania watano katika wiki ya kwanza ya Januari 2020.

“Nilishtuka kwa sababu idadi ya Watanzania waliokuwa wanakamatwa Guangzhou ilipungua katika miaka ya karibuni kulinganisha na 2016 hadi mwaka jana. Lakini kitendo cha kukamatwa kwa Watanzania watano wakiwamo wanawake wawili ndani ya mwezi mmoja tu, kimenishtua,” alisema.

Alisema miongoni mwa waliokamatwa ni mwanamke Mtanzania (jina halikupatikana) mwenye watoto watano ambaye alikamatwa Ethiopia, Januari mwaka huu.

Mtanzania mwingine alikamatwa Januari 7, 2020 akiwa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong na alipopelekwa hospitali alitoa gramu 980 za cocaine alizomeza. Hati ya kusafiria ya Mtanzania huyo ilionyesha ametokea Ethiopia.

Mtanzania mwingine ambaye jina lake lilitajwa kuwa ni Moses Maembe, alikamatwa Agosti 20, 2019 akiwa amebeba gramu 604 za cocaine, naye akiwa ametokea Addis Ababa.

Agosti 21 alikamatwa Mtanzania mwingine anayeitwa Peter Ndunguru akiwa amebeba gramu 804 za cocaine na hati yake ya kusafiria ikionyesha ametokea Ethiopia, akielekea Macau.

Watanzania wengine wanne waliokamatwa Hong Kong walikuwa wametokea Ethiopia isipokuwa mwanamke mmoja ambaye hati yake ilionyesha ametokea Dubai.

Mwingine ni Julieth Ngereza, Mtanzania aliyekamatwa Oktoba 31, 2019. akiwa amemeza gramu 600 za cocaine na ambaye hati yake ilionyesha ametokea Lusaka, Zambia.

Kwa mujibu wa Padri John, kwa sasa Watanzania walio magerezani nchini China ni 130 na wanasubiri kunyongwa.

“Hong Kong si China, ila ni sehemu ya China, lakini ina utawala tofauti na wenye sheria zake. Nchini China, sheria inasema anayekamatwa na dawa za kulevya ananyongwa na Watanzania wengi wanasubiri kunyongwa huko,” alisema

Padri Wootherspon alisema ameamua kuja Tanzania kuwakanya wananchi kuhusu hatari ya kupelekwa Ethiopia na watu wasiowafahamu kwa undani.

“Lakini zaidi kuwaeleza Watanzania kuwa kwa sasa raia wa Nigeria, wanawasaka Watanzania walio na shida ya ajira kusafirisha dawa na mara nyingi wanawake,” alisema.

“Lakini zaidi natamani Serikali ya Tanzania isaini makubaliano ya kuhamisha wafungwa walio China na Guangzhou warudi Tanzania,” alisema.

Maisha ‘bora’ gerezani

Ingawa Padri Wotherspon amesema anatamani kuwe na mbadilishano wa wafungwa, asilimia 90 ya wafungwa wa Kitanzania walio magerezani hawataki kurudi.

Hiyo ni kwa sababu maisha ndani ya magereza ya Hong Kong yana unafuu. Kwa mfano, Padri John alisema, wafungwa wenye uwezo wa kufanya kazi, kama kushona, kuunganisha vitabu, kudarizi, seremala wanalipwa kati ya Sh115,000 na Sh185,000 kwa mwezi.

Si hilo tu, bali wanapata bure matibabu ya magonjwa yote, ikiwamo upatikanaji wa dawa zote za saratani na Ukimwi.

“Wafungwa hao hupata nguo mpya kila mwezi na viatu, pamoja na kibali cha kusomea kozi mbalimbali, kuanzia cheti, diploma na shahada ya uzamili,” alisema.

Kuhusu chakula, Padri Wootherspon alisema wafungwa wanaweza kuchagua wanachotaka.

“Wengi wanaona nafuu kufungwa Hong Kong kwa kuwa wanaweza kufanya kazi na kupeleka fedha kwa familia zao Tanzania,” alisema.

Akizungumzia mbinu hizo mpya, aliyekuwa Kamishana wa Dawa za Kulevya nchini, Alfred Nzowa alisema kwa kawaida wafanyabiashara wa dawa hizo wanapoona mpaka mmoja umedhibitiwa hutafuta mwingine.

“Ni wajanja sana, na mipango yao haichukui siku, mbili ni ya muda mrefu,” alisema.

Alisema ili kuzuia Watanzania wasitumiwe kupitisha dawa hizo Ethiopia, Serikali inatakiwa kufanya ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Akiwa Kamishna wa dawa za kulevya, Nzowa alifanikisha kukamatwa kwa Khatibu Haji Hassan maarufu kama Shikuba, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 99 jela nchini Marekani. Shikuba alihukumiwa pamoja na Watanzania wengine tisa.