Polisi Tanzania wataka bendera za Chadema zishushwe

Muktasari:

olisi wafika eneo la ukumbi wa Mlimani City ambao Chadema wanakofanya mikutano yao na kuamuru viongozi wa chama hicho kushusha bendera walizoziweka kando kando barabara ya Sam Nujoma.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limefika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam likiwataka viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Tanzania (Chadema) kushusha bendera za chama hicho zilizowekwa barabara ya Sam Nujoma.

Bendera hizo zimewekwa kuanzia Superstar hadi mzunguko karibia na Kanisa na Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) ambapo chama hicho kinafanya mikutano ya uchaguzi katika ukumbi wa Mlimani City iliyoanza Desemba 9, 2019 na itahitimishwa keshokutwa Alhamisi ya Desemba 19, 2019

Askari polisi sita waliokuwa kwenye magari mawili aina ya Noah na Land Cruiser  waliutaka uongozi Chadema kushusha bendera hizo kwa maelezo kuwa ni amri kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic.

Mapema leo Jumanne Desemba 17, 2019 Dominic alikiandikia barua chama akikitaka kuzishusha bendera hizo zilizowekwa eneo la bustani pembezoni mwa barabara hiyo akieleza zimewekwa kama matangazo au mabango kinyume cha utaratibu.

Polisi hao walikutana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo, Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano  na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob,  Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika mazungumzo yao viongozi hao waligoma kuzishusha bendera hizo.

"Wametuambia tuzishushe halafu kesho tuzipandishe, tumewaambia hilo haliwezekani, labda washushe wao," amesema Jacob.

Naye Mrema amesema "Msimamo wa chama hatushushi bendera kwa sababu hatuvunji sheria kama chama cha siasa. Wakitaka wazishushe wao," amasema Mrema akiwaambia baadhi ya wanachama wa chama hicho waliokuwa wakisubiri mrejesho wa suala hilo.

Baada ya Mrema kutoa kauli hiyo baadhi ya wanachama walisikika wakiwahamasisha wenzao kutoka nje ya ukumbi kwenda barabarani kulinda bendera hizo.

Mpaka saa 2:30 asubuhi polisi walikuwapo eneo hilo huku baadhi ya wanachama wakienda barabara kulinda bendera hizo.