Polisi wamsaka dereva wa lori lililoua saba, kujeruhi

Tuesday September 10 2019

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Agostino

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Agostino Senga 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Simanjiro. Polisi Mkoa wa Manyara nchini Tanzania wanamtafuta dereva wa lori aina ya Fusso lililosababisha ajali iliyoua watu saba baada ya kupinduka mlima Namalulu wilayani Simanjiro mkoani humo wakati likienda mnadani.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Agostino Senga akizungumza leo Jumanne Septemba 10,2019 amesema wanamtafuta dereva huyo wa lori aliyetambulika kwa jina moja la Rashid.

Amesema dereva huyo alikimbia baada ya kutokea ajali hiyo jana Jumatatu saa 2 asubuhi kwenye kijiji cha Namalulu kata ya Naberera.

"Mara baada ya kutokea ajali hiyo dereva huyo alikimbia ila tunamtafuta huku tukiendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo na hatujabaini idadi ya abiria waliokuwa katika gari hilo," amesema kamanda Senga.

Hata hivyo, amesema baadhi ya ndugu wa marehemu wa ajali hiyo wameshatambua miili ya marehemu wawili na wanaendelea na taratibu za mazishi japo hakutaja majina ya waliotambulika.

Amesema ajali hiyo ilitokea kwenye Barabara Kuu ya Arusha- Orkesumet ambapo gari hilo aina ya Fusso lilikuwa limetokea jijini Arusha kwenda mnadani wilayani Simanjiro.

Advertisement

Amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana ila lilipinduka kwenye mlima wa Ngorika uliopo kijiji cha Namalulu wilayani Simanjiro.

 

"Liliacha njia na kupinduka ambapo watu watano walifariki dunia papo hapo na wengine wawili walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya Orkesumet," amesema

Amewataja waliofariki ni Leapa Lekara (31) na Aloyce Temba 32, wakazi wa jijini Arusha, Mosses Mgonja (31) mkazi wa Rombo Kilimanjaro, Chemana Shedrack (36) mkazi wa Sanawari jijini Arusha na Anna Kileo (46) mkazi wa Sanya juu mkoani Kilimanjaro.

"Marehemu wengine wawili bado majina yao hayajatambulika kwa haraka na majina ya majeruhi saba waliopelekwa Seliani na wale wa Orkesumet bado hatujapata kwa haraka," alisema kamanda Senga.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Dk Jesca Lebba amesema walipokea  miili ya marehemu hao saba na imehifadhiwa.

"Majeruhi wengine wamepelekwa hospitali ya Seliani jijini Arusha na wengine watano tunaendelea kuwapa matibabu ila wengine zaidi ya 30 wameruhusiwa kwani walikuwa na majeraha madogo," amesema Dk Lebba.

 

Advertisement