Prezzo atangaza kugombea ubunge

Muktasari:

Mwanamuzi huyo amejiunga katika chama cha upinzani cha Wiper kinachoongozwa na Makamu wa Rais wa zamani, Kalonzo Musyoka.

Nairobi, Kenya. Mwanamuziki wa Kenya, Jackson Makini maarufu Prezzo ametangaza kugombea ubunge katika Jimbo la Kibra jijini Nairobi, Kenya.

Mwanamuziki huyo maarufu nchini Kenya ametangaza kuwania nafasi hiyo kupitia chama cha upinzani cha Wiper kinachoongozwa na Makamu wa Rais wa zamani, Kalonzo Musyoka.

Prezzo alitangazwa kuwania nafasi hiyo leo asubuhi na makamu huyo wa Rais wa zamani mbele ya waandishi wa habari jijini Nairobi.

Prezzo anaungana na wanamuziki wengine maarufu wa Afrika Mashariki kuingia katika siasa za upinzani akiwamo Jose Chameleon na Bobi Wine (Uganda), Joeph Mbilinyi ‘Sugu’ na Joseph Haule ‘Profesa J’, Said Fela ‘Mkubwa fela’ na Ilaiton Chipande ‘Baba Levo’ (Tanzania) na Charles Njagua maarufu Jaguar (Kenya) ambaye kwa sasa ni mbunge wa Jimbo Starehe.

Uchanguzi wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Kibra unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge Ken Okoth kufariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kansa kwa muda mrefu.

Akizungumza katika utambulisho huo, Musyoka alisema anaimani mwanamuziki huyo atashinda nafasi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 7.

Prezzo, ambaye aliambatana wafuasi wake hasa vjana kutoka Kibra, aliahidi kutekeleza miradi ya maendeleo iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo .