Profesa Lipumba asema CUF haitasusia tena uchaguzi

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa gazeti la mwananchi, alipotembelea ofizi za Mwananchi Communication Limited, zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha wananchi (CUF) nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 huku akitoa sababu ya kwa nini chama hicho hakitasusia tena uchaguzi.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha wananchi (CUF) nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama chake kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019 kwa kusimamisha wagombea katika maeneo yote bara na visiwani.

Profesa Lipumba amesema hayo jana Jumatatu Septemba 23, 2019 alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

MCL ni wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika mahojiano hayo maalum, Profesa Lipumba alisema miongoni mwa mambo ambayo chama hicho hakiwezi kuthubutu kufanya ni kususia uchaguzi huku akitolea mfano wa mkulima kutosusuia shamba kisa mazao yake yanaliwa na nyani au wanyama wengi.

“Licha ya hali tete ya kisiasa tuliyonayo hatuwezi kususia uchaguzi, kususia sio dawa ya kuleta mabadiliko, tulifanya hivyo Zanzibar katika uchaguzi wa marudio mwaka 2015 na sasa hatuna mbunge wa baraza la wawakilishi hata mmoja wakati uchaguzi wa awali tulikuwa tumeshinda viti 27,” alisema Profesa Lipumba alipoulizwa endapo chama chake kinatarajia kushiriki uchaguzi.

Profesa Lipumba alisema wasingesusia uchaguzi huo chama hicho kisingeshiriki katika kuunga Serikali ya kitaifa lakini kwa kususia hakijapata nafasi hivyo kinakosa fursa hata ya kupinga mabadiliko ya Sheria mbalimbali katika baraza hilo akitolea mfano Sheria ya uchaguzi inayotaja siku mbili za kupiga kura (siku ya watumishi wa vyombo vya dola na siku ya wananchi).

Alisema ana imana endapo haki itatendeka chama hicho kitafanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo kuliko uchaguzi uliopita kwa kuwa mazingira sasa yamebadilika na chama kimeboreshwa zaidi.

Alisema mpaka sasa hawajaamua kushirikiana na chama chochote katika chaguzi zijazo lakini kuna vyama vimeleta mapendekezo (akikataa kuvitaji) ambayo yanajadiliwa kuona kama wanaweza kushirikiana.

Undani wa mahojiano haya ikiwamo jinsi anavyomzungumzia aliyekuwa kiongozi mwenzake ndani ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyetimukia chama cha ACT Wazalendo na kugombea urais 2020 usikose Gazeti la Mwananchi kesho Jumatano Septemba 25,2019