Profesa Tibaijuka aaga bungeni akiwa na uchungu wa sakata la Escrow

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Profesa Anna Tibaijuka akiwaaga Wabunge baada ya kumaliza kuchangia bungeni leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Muleba Kusini Nchini Tanzania (CCM), Profesa Anne Tibaijuka ameliaga Bunge kuwa hatagombea tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Dodoma. Mbunge wa Muleba Kusini Nchini Tanzania (CCM) Profesa Anne Tibaijuka ameliaga Bunge rasmi kuwa hatagombea tena ubunge na kukabidhi serikalini hoja yake binafsi aliyoipigania kuingia bungeni kwa miaka 10 bila mafanikio.
Profesa Tibaijuka ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 3, 2020, wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2020/2021.
“Kwa kupitia ofisi yako nakushukuru kuwa umemwandikia mheshimiwa Jenista Mhagama kumkabidhi hoja yangu binafsi ambayo nimehangaika nayo tangu Bunge la 10,”amesema.
Amesema kwa rekodi ya kumbukumbu rasmi za taarifa za Bunge ionyeshe kuwa amemkabidhi Jenista hoja yake binafsi.
Amesema hoja hiyo ilikuwa inazungumza baada ya kukumbwa na tatizo la Escrow alijikuta anahukumiwa na Bunge akiwa ndani ya Bunge lakini hakuruhusiwa kusimama kujitetea.
“Nikaona kuwa tuna upungufu mkubwa wa mfumo wetu, nikaja na muswada binafsi Bunge la Makinda (Spika wa Bunge la 10 Anne Makinda) muda haukupatikana lakini nashukuru Bunge lako muda haukupatikana lakini angalau umepiga hatua na kukabidhi serikalini.
Amesema kazi ya mbunge ni kutunga sheria na si kujadili sheria zinazoletwa na sheria na kwamba ni jambo la msingi katika demokrasia.
“Nawashukuru sana wananchi wa Muleba Kusini kwa kunipa nafasi ya kuwa kwenye jimbo hili kwa miaka 10 nimejifunza mengi, naenda kuandika vitabu,”amesema.