VIDEO: RC Chalamila awarudisha nyumbani wanafunzi 392, awataka kulipa Sh200,000

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameamuru wanafunzi 392 wa kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kurudi nyumbani hadi Oktoba 28, 2019.

Mbeya.  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameamuru wanafunzi 392 wa kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kurudi nyumbani hadi Oktoba 28, 2019.

Amesema siku watakaporejea shuleni wanatakiwa kuwa na Sh200,000 kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni mawili ya shule hiyo yanayodaiwa kuchomwa moto na baadhi yao.

Ametoa uamuzi huo leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 baada ya kufika katika shule hiyo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, siku moja baada ya kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa shule hiyo kwa madai ya kuchoma moto mabweni ya shule hiyo.

Aliwacharaza viboko jana Alhamisi Oktoba 3, 2019 baada ya kufika shuleni hapo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Chunya na kupewa taarifa za wanafunzi 19, wakiwemo watano wanaoshikiliwa na polisi kwamba baada ya kukutwa na simu, saa chache baadaye mabweni mawili ya shule hiyo yaliungua moto.

Chalamila amesema wanafunzi ambao hatatekeleza  amri yake ya kulipa fedha  kupitia benki na  kutofika shuleni Oktoba 18, 2019, atafuatwa nyumbani kwa pingu na hataruhusiwa kufanya mtihani wake wa  mwisho.

Leo Chalamila amesema wanafunzi 14 aliowachapa viboko jana ambao pia walikutwa na simu watatakiwa kulipa Sh500,000 na watakaporejea shuleni waambatane na wazazi wao, kutaka fedha zote zipelekwe benki kabla ya Oktoba 18, 2019 na kupeleka risiti za malipo shuleni.

Baada ya kufika shuleni hapo aliwaita wanafunzi na kuwaeleza kuwa wamekuwa watovu wa nidhamukwa kutumia simu kinyume na taratibu na pia mabweni yaliyoungua moto ndio walikuwa wakiyatuma, hivyo hawana sehemu ya kukaa.

“Kwa kuwa walichukua uamuzi wa kuchoma mabweni baada ya simu zao kuchukuliwa, hii (kurudishwa nyumbani) ni sehemu ya adhabu yao.”

“Nimetafakari sana nyinyi mliochoma mabweni, na pia mnamiliki simu na mnatengeneza vifaa vya kuchaji simu ambavyo ni hatari na vinaweza kusababisha moto. Mnajigeuza mafundi kama mna hamu ya kuchoma moto, nendeni mkachome nyumba za baba zenu,” amesema Chalamila.

Ameongeza, “Kuanzia sasa wanafunzi wa kidato cha tano na sita mtaondoka kurudi kwenu, kuna watu wanang’ang’ana  hapa mtakung’utwa kichapo cha kufa mtu kwa sababu huo ni utovu wa nidhamu.”

“Na walimu wanaofundisha kidato cha tano na sita mtakwenda likizo kidogo, mkapumzike kidogo.”