RC Hapi amtaka Mchungaji Msigwa kueleza utekelezaji wa ilani ya CCM

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ali Hapi akizungumza katika mkutano wa Jimbo la Isimani

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi amelitaka jimbo la Iringa Mjini ambalo mbunge wake ni Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kufanya mkutano wa jimbo kueleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kama alivyofanya mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi ameagiza kufanyika kwa mkutano mkuu wa jimbo la Iringa Mjini ili wananchi wapewe taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema jimbo hilo linaloongozwa na mbunge wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa linatakiwa kufanya mkutano huo kama alivyofanya mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 21, 2019  Hapi amesema Serikali imetekeleza shughuli nyingi za maendeleo katika jimbo hilo ikiwamo ujenzi wa stendi ya mabasi ya Mkoa iliyogharimu Sh3.7 bilioni lakini kwa sababu linaongozwa na upinzani  hakuna mkutano ulioitishwa.

Hapi amesema hayo katika mkutano wa jimbo  ulioitishwa na Lukuvi kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.

“Ilani ya uchaguzi ya CCM imetekelezwa kwa kiasi kikubwa hata hapa Iringa mjini, kwa hiyo kuna haja ya kuitisha mkutano wa jimbo kama huu ili wananchi wajue kazi zilizofanyika, na hili lifanyike kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.”

“Tunataka wabunge wa Iringa kufanana na Lukuvi kwa kuwaambia wananchi kazi zinazofanyika, mbunge asiyefanya kazi anaharibu taswira ya CCM.”

Awali Lukuvi alisema wakati anapotekeleza kazi za jimbo hilo huwa hatumii kofia yake ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Kwa hiyo hata migogoro ya ardhi kwenye maeneo yenu tumieni njia zinazotakiwa kufikisha malalamiko ikiwemo kupitia kwa wakuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na baadaye wizarani,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema japo haruhusiwi kuuliza maswali bungeni kwa sababu ya nafasi yake ya uwaziri lakini amekuwa akijitahidi kutatua changamoto za jimbo hilo kama kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema imekuwa rahisi Serikali ya wilaya hiyo kutatua changamoto za jimbo la Isimani kutokana na ushirikiano uliopo baina ya mbunge na wananchi.