RC Mtwara ataja wanaokwamisha wafanyabiashara, wawekezaji

Wednesday September 25 2019

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RC) nchini Tanzania,

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RC) nchini Tanzania, Gelasius Byakanwa 

By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RC) nchini Tanzania, Gelasius Byakanwa amesema changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji zinasababishwa na baadhi ya watendaji waliopewa nyadhifa katika maeneo mbalimbali kushindwa kuzitatua.

Byakanwa ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 25, 2019 wakati akifungua mkutano uliowakutanisha mawaziri sita, watendaji wa sekta binafsi na umma na baadhi ya wafanyabiashara kwa ajili ya kufahamu changamoto zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara mkoani humo ili kuzitafutia ufumbuzi.

Amewataka wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi wote kujadiliana kwa uwazi ili kupata suluhu juu ya changamoto za kibiashara zinazowakabili kwa kuibua mijadala yenye tija ambayo matokeo yake yatachochea ukuaji wa biashara na uwekezaji mkoani humo.

“Matokeo ya mjadala huu yanaweza kusaidia kurekebisha sera au sheria, tukitambua kwamba moja ya changamoto ambazo tunayo kama Taifa ni utendaji wetu wa kimazoea,.”

“Kwa sehemu kubwa changamoto ambazo nimezisikiliza kutoka kwa wafanyabiashara zinakwamishwa sana na utendaji wetu waliopewa nyadhifa mbalimbali,” amesema Byakanwa

 

Advertisement

Amewataka wafanyabiashara na wawekezaji mkoani humo na kueleza meza kuu imejiandaa kuwasikiliza zaidi na kuwataka kueleza yale ambayo pengine serikali haijayaona au yale ambayo yamo na wanafikiri yanawakwamisha na kuikwamisha serikali kupata mapato.

 

Akizungumza mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mtwara, Said Swallah amesema zipo changamoto zinazotakiwa kufanyiwa kazi baina ya serikali na sekta binafsi na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ambazo ni changamoto za kitaasisi, utendaji, uendeshaji, mazingira na changamoto za kimamlaka.

Amesema katika kufikia hatua za kuyapatia ufumbuzi matatizo na changamoto zitakazowasilishwa zinaweza kufanyika kwa kufuata ngazi mbalimbali.

Swallah amesema suala mojawapo ni kusimama kwa muda mrefu utekelezaji wa miradi katika sekta ya gesi asilia hali inayopoteza matumaini ya wafanyabiashara wengi walioitikia wito wa serikali kuchangamkia fursa ya uwepo wa miradi mikubwa ambayo iliibuka na kutekelezwa kati ya mwaka 2010 hadi 2014.

“Hali imebadilika ghafla hata ukifanya ufuatiliaji wa karibu kwa kuangalia viashiria vya kuathirika kwa biashara katika mkoa unaweza kubaini ni kwa kiasi gani baada ya kusimamia kwa shughuli za uwekezaji katika sekta ya gesi na mafuta zinaonekana bayana, moja kati ya maeneo hayo ni sekta hiyo ni hoteli na nyumba za kulala wageni,”amesema Swallah

Amesema hizo ni miongoni mwa sekta zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na baadhi yao wapo katika migogoro na benki walizokopa kwa ajili ya kuwekeza wakiwa na matumaini kwamba fursa walizoelekezwa waichangamkie imeingia Mtwara.

Advertisement