Rais Lungu atoa neno kwa wafanyabiashara wadogo wa Tanzania, Zambia

Muktasari:

  • Kituo maalum cha huduma kwa pamoja cha Tunduma, Nakonde kimejengwa kwa gharama ya Sh14 bilioni kwa msaada ya wahisani kupitia shirika la Trade Mark East Africa.

Dar es Salaam. Rais wa Zambia, Edgar Lungu amesema maboresho ya biashara kati ya nchi yake na Tanzania yanawalenga wafanyabiashara wadogo ambao ndiyo wengi.

Akizungumza leo Jumamosi Oktoba 5, 2019 katika uzinduzi wa kituo maalum cha huduma kwa pamoja cha Tunduma, Nakonde mkoani Songwe akisema, kituo hicho kitarahisisha upitishaji wa mizigo na watu kwa nchi hizo mbili.

“Serikali hizi mbili hazikuchukua tu hatua za kusaidia wafanyabiashara wakubwa bali pia wadogo wanaovuka mipaka,” amesema Rais Lungu.

“Hii ni muhimu kwa sababu watu wengi wanategemea biashara ndogo na kwa upande wa Zambia, watu wengi wanaounga mkono chama chetu ni wafanyabiashara wadogo. Wafanyabiashara wakubwa wanakuja na kuondoka, lakini wadogo wanabaki. Lazima tuwasaidie sana.”

Ameendelea kusema tangu walipotia saini mkataba wa kuundwa kwa kituo hicho Juni 7, 2010 kumekuwa na maendeleo makubwa ili kiaze kufanya kazi.

“Hivi karibuni kimekuwa kikifanyiwa majaribio ya kusafirisha abiria. Bado hakijaanza kufanya kazi kwa ajili ya mizigo lakini kikianza kufanya kazi kitarahisisha usafirishaji wa mizigo.

Alisema mpaka wa Nakonde na Tunduma una shughuli nyingi kwa ukanda wa Kusini mwa Afrika ukihudumia zaidi ya magari 600 kwa siku.

“Kwa hiyo kuja kwetu hapa, ili tuweze kutekeleza maudhui ya kituo cha mpakani katika kuongeza ushindani wa ushoroba na utaongeza biashara kati ya nchi mbili,” amesema Rais Lungu.