Rais Magufuli amtaja Tundu Lissu, asema alitelekeza jimbo lake

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amempongeza mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu akisema jimbo hilo lilikuwa limetelekezwa na Tundu Lissu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amempongeza mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu akisema jimbo hilo lilikuwa limetelekezwa na Tundu Lissu.

Mtaturu amechaguliwa hivi karibuni kuwa mbunge wa Singida Mashariki kuchukua nafasi ya Lissu ambaye Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alitangaza kuwa amepoteza sifa za kuwa mwakilishi wa wananchi  wa jimbo hilo.

Akizungumza leo Jumatatu Septemba 16, 2019 katika hafla ya uzinduzi wa rada za kuongoza ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Rais Magufuli amewapongeza wajumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu pamoja na mbunge huyo wa Singida Mashariki, aliyemtaka akawatetee wananchi bila kujali vyama.

 “Nimefurahi kumuona hapa kwenye Kamati ya Miundombinu mbunge wa CUF (hakumtaja jina), lakini pia na mheshimiwa nani yule wa lililokuwa jimbo lililokuwa limetelekezwa. Ni jimbo gani hili.”

Huku akikuna kichwa Magufuli amesema, “Lilikuwa la Tundu Lissu ameshika huyu (huku akimnyooshea kidole Mtaturu).”

Ameongeza, “Safi kabisa hongereni mpigie makofi na ameingia na kazi  nakuahidi Serikali yangu tutashughulikia maji katika jimbo hilo.”

Septemba 9, 2019 Mahakama Kuu ilikataa  maombi ya Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Ndugai  uliosababisha ubunge wake kukoma.

Ilisema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Akisoma uamuzi huo Jaji Sirillius Matupa amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na mahakama iteunge taarifa hiyo.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Baada ya uamuzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitangaza jimbo hilo kuwa wazi na Mtaturu kupita bila kupingwa baada ya washindani wake 12 kushindwa kurejesha fomu.