VIDEO: Rais Magufuli asema CCM walichangia mbunge Mwambe kuhamia Chadema

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema 'figisu' ndani ya CCM  zilisababisha  mbunge wa Ndanda (Chadema),  Cecil Mwambe kugombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema 'figisu' ndani ya CCM  zilisababisha  mbunge wa Ndanda (Chadema),  Cecil Mwambe kugombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 15, 2019 aliposimama njiani kuzungumza na wakazi wa Ndanda wakati akielekea Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

“Mbunge wenu huyu (Mwambe)  alikuwa mgombea wa CCM (mwaka 2015) anakubalika lakini kwa sababu ya figisu za watu wa huku (CCM) nataka nieleze ukweli mimi huwa napasuaga   tu wakaacha kumpitisha akaamua kuhama CCM."

"Kwa hiyo huyu ni wetu mlifanya makosa wenyewe na mnafahamu makosa ya kukosea kuchagua,” amesema Magufuli.

Amesema Mwambe alitakiwa awe mbunge wa CCM, alimuita mbunge huyo  azungumze kuhusu suala hilo.

Katika maelezo yake Mwambe amesema, "niligombea kupitia CCM mwaka 2015 niliongoza kura za maoni kwa kuwa nilikuwa sifahamu mfumo mzuri wa chama kipindi hicho kura zangu alipewa mtu mwingine na niliambiwa kura zangu hazikutosha.”

“Lakini Mungu alichagua niwe kiongozi wa Ndanda,  nilikwenda Chadema  nikashinda,  nina ahidi nitaendelea kushirikiana na wananchi wa hapa."

Baada ya Mwambe kueleza hayo Rais Magufuli amesema,  "wakati mwingine tunajicheleweshea maendeleo sisi wenyewe. Mtu anapendwa na wananchi, anakipenda chama lakini figisu za chama mnamnyima mtu anayetaka kushiriki. Hili liwe fundisho kwa wanachama na wananchi wa huku.”

“Mimi niligombea (waliojitokeza kupitishwa kuwania urais CCM mwaka 2015) na watu 42 wa CCM ila kiukweli mimi nilikuwa nakubalika hawakunifanyia mzaha wakanipitisha. Wanaokubalika msiwafanyie figisu hiki ni chama chetu wote.”

Ameongeza, "nimekusikia hata ninapokuona moyo wako umejaa CCM ninakuamini na kama upo tayari kuhamia CCM uhamie,  msimkate tena ninahitaji watu watakaonipa ushauri mzuri kwa kuwa tunaongea lugha moja inayofanana kama ilivyo kwa Nape (Nnauye-mbunge wa Mtama- CCM)."