Rais Magufuli asema ofisi ya CAG sio safi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Charles Kichere kusafisha ofisi hiyo akisema kuna uchafu si safi kama watu wanavyofikiri.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Charles Kichere kusafisha ofisi hiyo kwa kuwa sio safi kama watu wanavyofikiri.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumatatu Novemba 04, 2019 katika hafla ya kumuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na wateule wengine mbalimbali iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

“Kwa CAG mpya kasimamie hiyo ofisi, kuna baadhi ya watendaji wako wanapotumwa kukagua kwenye balozi wanalipwa fedha hapa na wanapofika kule kwa mabalozi napo wanaomba tena pesa,” amesema.

“Sitaki kuwataja hapa lakini ofisi ya CAG sio ‘clean’ kama mnavyofikiria, sasa nenda kachambue ukapange ‘position’ za watu wako ili mauchafu uchafu haya ukayasafishe,” amesema.

Rais Magufuli pia amemtaka CAG Kichere kutekeleze maagizo anayopewa na mihimili mingine bila kubishana nayo.

“Nakutakia kazi njema, usije ukaenda huko ukajifanya na wewe ni muhimili, mihimili ni mitatu tu, na umeiona hapa, kuna Mahakama, kuna Bunge na sisi wengine wa Serikali, nafasi yako ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hiyo mwenye Serikali yupo.” 

“Kafanye kazi zako vizuri za ukaguzi, bila kuonea watu, unapopewa kazi na mihimili mingine kama Bunge kaitekeleze, usibishane nao, wewe ni mtumishi” amesema Rais

“Kwa hiyo nenda ukasimamie kazi yako vizuri, mwenzako aliyekuwepo amemaliza kipindi chake cha miaka mitano, kwa hiyo kuanzia kesho nenda ofisini ukaanze kufanya kazi, kayatoe mauchafu yaliyoko hapo,” amesema. 

Hafla hiyo imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai  na viongozi wengine wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.