Rais Magufuli ateua wengine

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi nne, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Mkuu wa Chuo cha Maji.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi nne, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Mkuu wa Chuo cha Maji.
Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne Januari 21, 2020 na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.
Katika taarifa hiyo Msigwa anaeleza kuwa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza Januari 2, 2020  na walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
Rais Magufuli amemteua Profesa Maurice C.Y. Mbago kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Profesa Mbago anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.
Rais Magufuli amemteua Dk  Masatu Masinde Leonard Chiguna kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Dk Chiguna anachukua nafasi ya Profesa Ninatubu Mbora Lema ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na bodi kuvunjwa.
Rais Magufuli amemteua Profesa Zacharia Mabubu Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL). Profesa Mganilwa ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Rais Magufuli amemteua Mariam Alu Nkumbi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Dk Godwill George Wanga kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC). Kabla ya uteuzi huo Dk. Wanga alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Rais Magufuli amemteua Dk Adam Omar Karia kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji.