Rais Magufuli atoa tahadhari ugonjwa wa corona

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona akisema ni hatari zaidi kwa maelezo kuwa ni ugonjwa hatari na Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshatoa tahadhari.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona akisema ni hatari zaidi kwa maelezo kuwa ni ugonjwa hatari na Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshatoa tahadhari.

“Ugonjwa wa corona upo duniani na umekumba nchi nyingi. Kwa takwimu zilizopo zaidi ya watu 100,000 wameambukizwa  na inakadiriwa watu 4,500 wamepoteza maisha. Ni ugonjwa mbaya sana,” amesema Rais Magufuli.

Ametoa tahadhari hiyo leo Ijumaa Machi 13,2020 wakati akizindua  karakana ya kisasa ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) iliyojengwa kwa Sh8.5 bilioni kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani.

Rais Magufuli amesema ingawa ugonjwa huo umesambaa katika maeneo mbalimbali dunia bado Tanzania haujaingia, “lakini Taifa haliwezi likajiweka pembeni bila kuchukua hatua ambazo tayari zimeshaanza kuchukulia kupitia wizara husika. Ndugu zangu Watanzania ni vyema tukaendelea kuchukua tahadhari kwa nguvu zote. Ugonjwa huu unaua kwa haraka sana, tusipuuze hata kidogo, lazima tuchukue hatua za kujikinga.”

“Kwa wale wanaopenda kusafiri safiri sana, kama safari siyo ya lazima usisafiri. Nimeshatoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi  hatutatoa kibali cha watu kusafiri wanavyotaka, lazima kuwepo kwa sababu za msingi.”

Amesema Watanzania wanaopenda kusafiri mikoa mbalimbali na wanakutana na watu wasiowafahamu ni vyema kupunguza safari hizo.

“Tatizo lipo na tusipuuze,  zile tahadhari  tunazopewa ikiwemo kutoshikana na mikono tusizipuuze tuzizingatie. Tusiwaache viongozi wazungumze kila mmoja kwenye familia atoe tahadhari , vyuoni, jeshi na  kwenye ufasiri,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema ugonjwa wa corona unaharibu uchumi akisisitiza umuhimu wa watu kuzingatia tahadhari zinazotolewa akisema zikidharauliwa watu watakwisha.

“Hadi leo dawa haijapatikana,  wanatibu corona  kupitia  dalili,  ujumbe huu leo hapa Lugalo uwaguse Watanzania. Viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kwa kila imani waendelee kutuombea kutuepusha na janga hili,” amesema Rais Magufuli.