VIDEO: Rais Magufuli awaeleza wapigakura wa Mtama alivyomsamehe Nape

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaeleza wananchi wa jimbo la Mtama alishamsamehe mbunge wao, Nape Nnauye na anashirikiana naye katika ujenzi wa Taifa.

Lindi. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaambia wananchi wa jimbo la Mtama mkoani Lindi kwamba tayari alishamsamehe mbunge wa jimbo hilo, Nape Nnauye

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiwalala wakati akienda wilaya ya Ruangwa, leo Jumanne Oktoba 15, 2019 Rais Magufuli baada ya kumpa Nape nafasi ya kuzungumza aliwaambia ni kijana mnyenyekevu na mwenye kuelewa anachoelekezwa.

Baada ya hapo akizungumza na wananchi wa eneo la Mtama Rais Magufuli amerudia tena kauli hiyo akizidi kumsifia Nape na kuwashukuru wananchi kwa kura walizompa wakati wa uchaguzi mkuu 2015.

“Nawashukuru sana ndugu zangu kwa kura zenu mlizonipa niko na nyinyi, lakini pia niwashukuru kwa kura mlizompa kijana wangu (Nape),” amesema Rais Magufuli huku akimtazama Nape

“Si mnamuona kijana wangu mrefu, mzuri ni mnyenyekevu aliomba msamaha, tunaendelea kufanya kazi na ukimwambia kitu ni muelewa,” amesema

Nape alikwenda Ikulu Septemba 10, 2019 kumuomba Rais Magufuli msamaha baada ya kuvuja kwa sauti walizokuwa wakimsema.

Wengine waliiomba msamaha ni wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na William Ngeleja wa Sengerema.