Rais Magufuli awapiga ‘stop’ Ma Ded kukopa fedha

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapiga marufuku wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote nchini kutokopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha atakayefanya hivyo ajiandae kuachishwa kazi

Bukombe. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapiga marufuku Wakurugenzi  Watendaji wa Halmashauri zote nchini humo kuacha  mara moja kukopa fedha kwenye taasisi za fedha kwa madai ya kufanya miradi ya maendeleo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 27, 2019 wilayani Bukombe mkoani Geita wakati akihutubia mkutano wa hadhara, Rais Magufuli amewaagiza iwapo wapo ambao wameshachukua fedha hizo kuzirudisha na kuvunja mikataba waliyoingia.

“Kama kuna mkurugenzi yeyote amekopa fedha azirudishe, mwenye mamlaka ya kukopa kwa niaba ya Serikali ni paymaster general wa Serikali ambaye ni Wizara ya Fedha pekee.”

“Anayekopa ajiandae kutoka. Naamini Wakurugenzi wamenielewa, nimepita Kahama Mkurugenzi ananiambia anataka kukopa kutoka TIB (Benki ya Uwekezaji Tanzania) kwa ajili ya kujenga stendi, haiwezekani fedha za wananchi kuchezewa, ovyo”  amesema Rais Magufuli

“Mkurugenzi wa hapa yupo wapi? amehoji, wewe umekopa?, kumbe wewe ni mtu mzuri, waeleze na wenzako si mna magrupu ya WhatApp waambie kwamba ni marufuku kukopa kuanzia leo kutoka benki yoyote ile,” amesema