Rais Magufuli kuwaapisha viongozi wateule kesho

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli kesho anatarajia kuwaapisha viongozi wa wizara, mahakama, majeshi na mikoa aliowateua juzi kushika nyadhifa mbalimbali.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli kesho Jumatatu Februari 3, 2020, atawaapisha viongozi wa wizara, mahakama, majeshi na mikoa aliowateua juzi kushika nyadhifa mbalimbali.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ikulu Mawasiliano leo Jumapili Januari 2, 2020 ilieleza kuwa viongozi watakaoapishwa ni makatibu wakuu watano, naibu katibu mkuu mmoja, makatibu tawala wa mikoa watatu, kamishna jenerali wa magereza na kamishna jenerali wa zimamoto na uokoaji.

Wengine ni Kamishna wa ardhi wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania, msajili wa Mahakama ya rufani, msajili wa Mahakama kuu na wajumbe watatu wa tume ya utumishi wa Mahakama.

Viongozi hao wataapishwa kuanzia saa 3:15 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam na wanatakiwa kufikia Ikulu kabla saa 2:00 asubuhi kupitia lango la Mashariki (lango la baharini).