Rais Magufuli kuweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja Mwanza

Muktasari:

Leo Jumamosi Desemba 7, 2019-12-07, Rais wa Tanzania, John Magufuli ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi jijini Mwanza litakalokuwa na urefu wa kilomita 3.2 na litajengwa kwa muda wa miezi 48.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi Desemba 7, 2019 anaweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi mkoani Mwanza.

Licha ya mvua zinazoendelea kunyesha, tayari mamia ya wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania, dini na kisiasa wameshafika katika hafla inayofanyika eneo la Kigongo wilayani Misungwi.

Baadhi ya viongozi ambao wameshafika akiwamo Rais Magufuli ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na makatibu wakuu.

Vikundi vya ngoma na kwaya mbalimbali  vimetumbuiza kabla ya Rais Magufuli kuwasili.

Daraja hilo linalokatiza katika ziwa Victoria, kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Patrick Mfugale  litakuwa na nguzo 64 na litajengwa kwa gharama ya Sh582 bila VAT.

Litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 kutoka Kigongo wilayani Misungwi hadi Busisi wilayani Sengerema na litajengwa kwa miezi 48 sawa na miaka minne.

Daraja hilo litakalojengwa na kampuni mbili litakuwa na uwezo wa kupitisha mabasi, baiskeli, pikipiki na watembea kwa miguu.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojili