Rashford atungua mwishoni kuizamisha PSG

Muktasari:

Rashford amerudia miujiza yake aliyoonyesha mwishoni mwa mechi dhidi ya PSG katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 2019.

 

Paris, Ufaransa (AFP).Marcus Rashford jana Jumanne alifunga tena mwishoni mwa mchezo na kuizamisha Paris Saint-Germain wakati klabu yake ya Manchester United ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya washinda washindi hao wa pili wa msimu uliopita katika Uwanja wa Parc des Princes jijini Paris.

Mshambuliaji huyo wa England, ambaye penati yake aliyopiga katika dakika za mwisho iliipa United ushindi safi katika mechi ya hatua ya timu 16 bora mwaka 2019, jana alifunga bao katika dakika ya 87 wakati kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kilipopata pointi tatu kilizostahili katika mechi ya Kundi H.

Ulikuwa ni ushindi mtamu wa ugenini kwa klabu hiyo ya Ligi Kuu na kocha Solskjaer alifurahishwa kwa jinsi ngome yake ilivyowadhibiti washambuliaji watatu; Neymar, Kylian Mbappe na Angel Di Maria.

"Tulicheza dhidi ya timu nzuri na tulilazimika kujilinda vizuri. Wachezaji ndio walifanya vizuri. Sidhani kama kuna siri yoyote, tunahitaji kucheza vizuri ili kuishinda PSG," alisema.

Kocha huyo kutoka Norway aliamua kumchezesha kwa mara ya kwanza beki wa kushoto, Alex Telles wakicheza watatu katika ngome pamoja na Luke Shaw na Axel Tuanzebe.

"Tunajua ubora wa Axel, ni beki mzuri. Mechi yake ya kwanza katika miezi kumi ni ushuhuda wa ni beki wa aina gani," Solskjaer aliiambia BT Sport.

Kocha huyo wa United pia alimsifu Rashfor akisema mshambuliaji huyo "anapenda upande huo wa uwanja".

"Zote zilikuwa nafasi za kushinda mchezo. Kama mshambuliaji inapokuwa mwishoni, hiyo iko akilini, unaweza kupata nafasi moja na lazima ufanye kila uwezalo kufunga," alisema Rashford alipoongea na BT Sport baada ya kurudia maajabu aliyofanya misimu miwili iliyopita.

United ilipata bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliochezwa bila ya mashabiki jijini Paris, bao lililofungwa kwa njia ya penati na Bruno Fernandes.

Lakini ilionekana kama PSG ingeepuka kipigo kwa kupata sare baada ya Anthony Martial kuusukumia kwa kichwa golini kwake mpira wa kona iliyopigw ana Neymar dakika kumi baada ya kipindi cha pili kuanza.